Na Florah Temba, wa dev.kisakuzi.com-Moshi
ZAIDI ya watu 46,300 toka Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamebainika hawajui kusoma na kuandika hali ambayo imekuwa kikwazo kikubwa katika jitihada za kufuta ujinga na kukuza kiwango cha elimu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Campass ya Mbeya Dk. Ernest Kihanga wakati akiwasilisha taarifa ya Mpango Mkakati wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kwa kipindi cha Mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016 kwenye kikao cha wadau wa maendeleo wa halmashauri hiyo.
Alisema kulingana na tafiti walizozifanya katika halmashauri hiyo walibaini kuwa kumekuwepo na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika hali ambayo imekuwa ikichangiwa na wanafunzi kuacha shule pamoja na kujiingiza kwenye biashara wangali wadogo.
“Idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ni 46,308 ambapo wanawake ni 22,230 na wanaume ni 24,078,idadi hii ni kubwa sana hasa katika kipindi hiki ambacho nchi iko kwenye mipango ya kutokomeza adui ujinga,umaskini na Maradhi,” alisema.
Aidha alisema wanafunzi kuacha shule bado ni tatizo kubwa katika halmashauri ya wilaya ya Moshi na hali hiyo ni kutokana na utoro na mtazamo duni kuhusu elimu.
Wakizungumzia suala hilo la watu kutojua kusoma na kuandika baadhi ya wadau wa maendeleo katika wilaya hiyo walielezea kusikitishwa na idadi hiyo na kusema kuwa uwajibikaji wa walimu na wazazi bado haukidhi matakwa ya wanafunzi hivyo kuchangia vitendo vya utoro kuzidi kushamiri. Kutokana na hali hiyo wadau hao waliitaka jamii kuongeza nguvu katika kusaidiana na walimu ili kuweza kulisaidia taifa kuondokana na tatizo hilo la wimbi kubwa la watu wasiojua kusoma na kuandika.
“Kimsingi ni kwamba hili ni tatizo kubwa katika taifa na kwa kiasi kikubwa linachangiwa na wanafunzi kujiingiza katika vitendo viovu kama vile uvutaji wa madawa ya Kulevya na vya ngono wakiwa wadogo hali ambayo inawaharibu na kuwafanya wajisahau katika masomo”alisema Bw.Koeli Shayo mmoja wa wadau hao.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Juliana Malange alisema halmashauri hiyo itashirikiana kwa karibu na wadau ili kuhakikisha mpango mkakati wa maendeleo unafanikiwa kwa kiwango cha juu.