Madereva daladala wagoma Moshi

Na mwandishi wetu Moshi

MADEREVA wa magari madogo maarufu kama Hiace yanayofanya safari zake katika mji wa Moshi jana wamegoma kwa muda usiojulikana wakilalamikia halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuwapandishia ushuru kutoka Sh. 1,000 hadi 1,500 pamoja na jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani kuwaomba rushwa.

Madereva hao wanaofanya safari za Kiboriloni,Pasua, Majengo,Soweto na KCMC ndani ya manispaa ya Moshi waliegesha magari yao katika eneo la Manyema na kuanza kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya mji wa moshi huku wakipiga kelele Kero kero hali ambayo imesababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa manispaa hiyo hususani wafanyabiashara na waliokuwa wanakwenda kutazama wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika eneo la Manyema kata ya Bondeni baadhi ya madereva hao walisema kitendo cha halmashauri ya manispaa ya Moshi kupandisha ushuru kutok a 1,000 hadi 1,500 ni cha unyanyasaji kutokana na kwamba wameonekana kufanyia kazi watu badala ya kujiendeleza wao.

Walisema pamoja na ushuru huo wa sh. 1,500 wamekuwa wakitakiwa pia kulipa sh. 10,000 kwa ajili ya ushuru wa maegesho,sh.291,000 kwa mamlaka ya mapato nchini (TRA)kwa mwaka, Sh. 150,000 kwa ajili ya ukaguzi,35,000 sumatra,hivyo mwisho wa siku kujikuta wakiishi katika mazingira magumu ili hali wanafanya kazi kila siku.

“Tunaiomba manipsaa isikilize kilio chetu na kupunguza ushuru huu kwani ni mkubwa sana ikilinhganishwa na fedha tunazozipata na hata ikiwezekana wawaondoe mawakala katika kazi hii na halmashauri iwe inapokea fedha hizi yenyewe kwani hapa wakala anataka faida yake na halmashauri haiambulii chochote “alisema Laurance Ngoti .

Malalamiko mengine ya dereva hao ni kuombwa rushwa na Askari wa kikosi cha usalama barabarani ambapo walisema wamekuwa wakipata usunmbufu mkubwa barabarani kila siku hali ambayo imewafanya kushindwa kusonga mbele kimaendeleo kutokana na kwamba fedha ambazo wamekuwa wakifanyia kazi nyingi zimekuwa zikiishia polisi.

Walisema askari wa kikosi cha usalama barabarani(Trafic) huwataka wawape Sh. 1,000 hadi 2,000 kila wanapowasimamisha ambapo kwa siku huweza kuwakamata hadi mara Nne hali ambayo inawaumiza sana hasa ikizingatiwa kuwa mara nyingi wanakamatwa wakiwa hawana makosa.

Kufuatia mgomo huo kiliitishwa kikao cha dharura cha viongozi wa wasafirishaji na halmashauri ya manispaa ya moshi ili kuweza kuongelea na kujadili matatizo hayo kutokana na kuonekana kuwepo kutoelewana baina ya viongozi wa manispaa waliofika eneo la Manyema na madereva.

Hata hivyo baada ya kikao hicho majibu hayakuweza kutolewa moja kwa moja na badala yake halmashauri ya manispaa ya Moshi iliwaomba viongozi wa madereva hao wakutane na madereva na wawaombe kurudi kazini hadi Tarehe 25 ambapo ndipo majibu ya kero zao yatatol.ewa.

“Tumewapomba viongozi wa madereva hawa wakakutane nao na kuwataka warudi kazini pindi tunapoendelea kushughulikia matatizo yao kwani ni mengi na mengine ni makubwa hatuwezi kuyatolea majibu leo, hadi tarehe 25 ambapo tutakutana tena na viongozi hawa ili tutoe majibu”alisema Mstahiki Meya wa manispaa ya Moshi Bw. Jafari Michael.

Naye kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro Bw. Robert Boaz alikiri kuwepo kwa mgomo na kusema kuwa kikubwa kinacholalamikiwa ni Ushuru na kwamba kuhusiana na Trafic kuomba rushwa bado hana taarifa na hivyo atalishughulikia.

Alisema kwa sasa milango ya Polisi iko wazi na kama kunadereva ambaye anaombwa rushwa na trafic afike kutoa taarifa ili hatua zingine zichukuliwe na kwamba cha msingi ni kila mmoja azingatie sheria na taratibu za usalama barabarani.