Afungwa maisha kwa kumuua Malkia

Mahakama ya kimataifa inayochunguza mauji ya kimbari nchini Rwanda{ICTR} imemhukumu mwanajeshi wa zamani kifungo cha maisha jela kwa kuhusika na mauaji hayo ya mwaka 1994.
Ildephonse Nizeyimana,alipatikana na hatia ya kuamrisha mauaji ya aliyekuwa Malkia wa jamii ya Tutsi Rosalie Gicanda pamoja na mauaji mengine.Nizeyimana alikamatwa nchini Uganda mwaka wa 2009.
Aliongoza kitengo cha ujasusi na operesheni za jeshi katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha ESO,wakati wa mauaji ya kimbari.
Mahakama hiyo iliyoko mjini Arusha, Tanzania ilimpata na hatia mwanajeshi huyo wa zamani ambapo aliamrisha mauaji ya raia kadhaa akiwemo malkia huyo wa Tutsi.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch mwaka wa 1999, wanajeshi wa Ki-Hutu walimchukua Malkia huyo kutoka makaazi yake Kusini Mashariki katika mji wa Butare na kisha kumpiga risasi nyuma ya jumba la makumbusho.
Pia waliwaua wanawake wakadhaa waliokuwa wajakazi wa malkia huyo.Marehemu alikuwa mjane wa Mfalme Mutara III, aliyefariki dunia mwaka wa 1959 kabla ya nchi hiyo kutangazwa jamuhuri.
Mahakama ya ICTR ilibuniwa kuwafungulia kesi wafadhili na washiriki wa mauaji ya kimbari. Tayari imewahukumu watu 54 na kuwaachia huru wanane. Mahakama hiyo inafunga shughuli zake baadaye mwaka huu.

-BBC