Mhariri Willy Edward Buriani kazi zako zitakumbukwa daima.

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinaungana na familia, wafanyakazi wa Jambo Leo, Jukwaa la wahariri, wanahabari na Watanzania wote kuombeleza kifo cha Mhariri Mkuu wa Jambo Leo Willy Edward ambaye alifanya kazi zake kwa umakini wa kupigiwa mfano.

Sisi TAMWA tunautambua na tunauenzi mchango mkubwa wa marehemu Willy Edward katika kuhakikisha kuwa gazeti la Jambo Leo linafanya tafiti na kuchapishwa habari zenye kuelimisha na kuhamasisha umma kutokomeza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu kwa wanawake na watoto nchini.

Vitendo hivyo ni pamoja na watoto wa kike kukatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa, vipigo kwa wanawake, ubakaji, wanawake na watoto kutelekezwa na mimba mashuleni ambavyo kwa kiwango kikubwa vinachangiwa na ulevi na kuendekeza ubaguzi kati ya wanawake na wanaume.

Mhariri Willy kwa namna ya pekee alizipa nafasi kwenye gazeti la Jambo Leo habari zilizolenga kuelimisha umma madhara ya vitendo vya ukatili na alitumia nafasi yake kama mhariri kuandika tahariri zinazokemea maovu hayo kwa kuwa aliamini kuwa amani, umoja na mshikamano wa familia ni chachu ya maendeleo ya familia na taifa zima.

Tunawapa pole Wahariri wote nchini kwa kuondokewa kwa gafla na mhariri kijana ambaye aliifanya kazi yake kwa ujasiri, umakini na mapenzi makubwa kwa taifa lake.

Tunalishauri Jukwaa la Wahariri nchini lianzishe mfuko wa kutunza afya za wahariri ili inapotokea mhariri kuhitaji msaada wa kugharimia matibabu nyeti kama vile yanayohusu magonjwa ya moyo aweze kupata kwa urahisi kutoka kwenye mfuko huo.

Aidha tunawaasa Wahariri na wanahabari wote nchini kufanya kazi zao kwa bidii, ubunifu, uadilifu na kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya habari kwa sababu kazi iliyotukuka siku zote hubaki ikikumbukwa hata kama aliyeifanya atakuwa amekufa.

Tunaamini kazi nzuri alizozifanya marehemu Willy na mema yote aliyowatendea watu mbalimbali vitaendelea kubaki vikikumbukwa.

Tunamuomba Mungu ailaze kwa amani mahali pema peponi roho ya marehemu Mhariri Willy Edward na kuwapa nguvu na roho ya subira wote walioumizwa na kifo chake. AMEN