Wanaharakati waichambua Bajeti 2012/13

Na Mwandishi wetu
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) unawakutanisha wanaharakati wa ngazi ya jamii, mashirika ya kijamii kujadili na kuchambua Bajeti ya mwaka wa fedha 2012/13 inayoendelea kujadiliwa Bungeni.
Bajeti ya mwaka wa Fedha 2012/13 ilisomwa Bungeni na waziri wa Fedha Wiliam Mgimwa, Juni 14 mwaka huu ikiwa na makadirio ya jumla ya shilingi Trilioni 15 kutoka Trilioni 13 za mwaka wa Fedha 2011/12.
Wanaharakati hao, kutoka Mikoa ya Ruvuma, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Dodoma, Arusha, Pwani na Dar es salaam, wanaungana na wanaharakati kutoka mashirika ya HAKIARDHI, ActionAID, NEDPHA,Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM), na vikundi vya kijamii(CBOs).
Mchambuzi wa sera na utafiti wa TGNP, Gloria Shechambo ameeleza kuwa nia na malengo ya kukutana ni kuaangalia Bajeti iliyotangazwa na serikali kama inabeba masuala ya wananchi wote hasa walioko pembezoni kwa mtazamo wa KIjinsia na baadaye watakuja na mawazo na maoni mbadala.
“Tunakutana hapa ili kujengeana uelewa na kuchambua kwa pamoja bajeti ya Taifa 2012/13, kuoanisha yaliyojiri kwenye bajeti na hali halisi ya kimuktadha, tuliyonayo na hali halisi ya wanawake hususani kutoka katika maeneo matatu, ambayo TGNP ilifanya utafiti raghibishi hivi karibuni”amesema Shechambo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu mallya alisema kuwa wananchi wote wanatakiwa kuelewa mchakato wa kuandaa bajeti ya kitaifa kuanzia ngazi za kijiji au mtaa na kuhakikisha vipaumbele vyao vinapitishwa kwenye Bajeti.
Mallya amesema kuwa ni muhimu kwa wanajamii kuunganisha nguvu zao kwa kujiunga kwenye vikundi vya kijamii, ili kudai haki zao ikiwemo kushiriki kwenye mikutano ya kijiji inayoitishwa ili kuleta mabadiliko.
Ameongeza kuwa mkutano huo wa siku mbili utaongozwa na Kikundi kazi cha uchambuzi wa Bajeti (BATT) kwaajili ya kutoa msimamo wa madai ya pamoja juu ya yanayojiri kwa mrengo wa ukombozi wa mwanamke kimapinduzi.
Aidha amesema kuwa wanaharakati hao watajenga mpango mkakati wa ufuatiliaji wa rasilimali katika maneo mbalimbali hasa sehemu wanazotoka.