WAKIONGOZWA na mchezaji ambaye ni vigumu kumkaba, Lionel Messi Timu ya Barcelona jana waliifanya vibaya Timu ya Manchester United baada ya kuichapa bao 3-1 katika fainali ya Klabu Bingwa Barani Ulaya.
Wakicheza kwa kujiamini na kulishambulia watakavyo lango la Manchester, wachezaji wa Barcelona walimfanya mchezo wa jana kuonekana wamewazidi wapinzani wao kila idara hivyo mchezo kuonekana ukichezwa upande mmoja.
Pedro mbele ya mashabiki zaidi ya elfu 87 walioshuhudia mpambano huo alianza kuwanyanyua mashabiki wa Barcelona dakika 27 baada ya kuiandikia timu hiyo goli la kwanza, ambalo lilidumu kwa muda mfupi kabla ya mchezaji hatari wa Manchester United, Wayne Roney kusawazisha goli hilo dakika ya 34 ya kipindi cha kwanza.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote zilikuwa na bao moja moja, japokuwa Man’United alionekana kuzidiwa kutokana na kushambuliwa muda wote wa kipindi hicho.
Lionel Messi ndiye mchezaji aliyevunja ukimya wa mashabiki wa timu hiyo baada ya dakika ya 54 kufunga goli la pili kwa kiki kali lililopigwa kwa kushtukizwa na kumshida golikipa wa Man’United,Edwin Van der Sar.
Kipigo cha Mashetani wekundu jana hakikuishia kwa Messi kwani, David Villa aliandika bao la tatu dakika ya 69 alilolifunga kwa ufundi mkubwa hivyo kupoteza kabisa matumaini ya Man’United kutwaa ubingwa huo. Hadi mwisho wa mchezo huo Barcelna 3 na Man’United wakiambulia goli moja (1).
Katika mchezo huo Barcelona iliwakilishwa na; Valdes, Dani Alves (Puyol 88), Mascherano, Pique, Abidal, Xavi, Busquets, Iniesta, Villa (Keita 86), Messi, Pedro (Afellay 90). Manchester United iliwakilishwa na Van der Sar, Fabio Da Silva (Nani 69), Ferdinand, Vidic, Evra, Valencia, Carrick (Scholes 76), Giggs, Park, Rooney, Hernandez.