Vikosi vya timu nyingi zinazoshiriki Euro 2012 vina mchanganyiko wa watu wenye asili tofauti, jambo ambalo Ulaya ya zama hizi inatakiwa izowee.
Yapo mengi ya kuvutia kuhusu mpira wa miguu barani Ulaya kwa sasa, lakini hili la watu wa asili ya nje ya Ulaya linaonekana kuwatumbua nyongo Wanazi mamboleo na wanaowachukia wahamiaji.
Ni bahati mbaya pia kwamba hili limefufuka kwa kuibukia kwenye siasa za Ulaya na dalili zake zimeanza kubainika kwenye viwanja vya soka barani.
Ama kwa hakika, mashindano ya Euro 2012 yanayokutanisha timu 16 bora za mataifa ya Ulaya nchini Poland na Ukraine kuanzia mwezi huu, sasa ni kumbusho kwamba maadui bado ni sehemu ya soka ya Ulaya.
Katika mashindano haya makubwa yanayoendeshwa kwa mtindo unaokaribia ule wa Fainali za Kombe la Dunia, tayari familia za wachezaji wawili weusi wa England zimevunja ratiba zao.
Familia za Theo Walcott na Alex Oxlade-Chamberlain zimeamua kutosafiri na wana ndinga hao kwenda Ukraine, kwa hofu ya uwezekano wa kulengwa na wahuni walioahidi kushambulia wageni.
Serikali ya Uingereza imewaonya raia wake juu ya hatari hii, na baadhi ya watu maarufu kwenye soka wameeleza wasiwasi wao juu ya hatari hio ya ubaguzi.
(Baba yake Chamberlain, Mark, alikuwa mmoja wa wachezaji wa kwanza weusi kuiwakilisha England, ikiwa ni zama zile ambapo ilikuwa kawaida kwa wanasoka weusi kushambuliwa kibaguzi na washabiki.)
Kuna tangazo fulani linalofurahisha, kwa sababu linaonyesha kuwapo jambo zuri na la maana sana kwenye kandanda barani Ulaya hivi sasa. Hilo ni tangazo la Nike linalowahusu wasakata soka kadhaa.
Kwa upande mmoja, tangazo hilo linaenzi mkusanyiko wa kumbukumbu ya soka duniani – kupitia mitindo maarufu ya nywele.
Inavyotokea ni kwamba, Mario Balotelli anamkatalia kinyozi mitindo yote hiyo, kabla ya kujituliza kwa aina yake mwenyewe ya mtindo wa ‘fauxhawk’.
Kwa yeyote ambaye amekuwa akifuatilia soka kwa miongo miwili iliyopita, hataacha kujua kwamba mtindo wa nywele wa ‘jheri’ si wa mwingine bali wa mchezaji asiyeweza kuigwa, Ronaldinho.
Mfuatiliaji gani makini atashindwa kung’amua kwamba kunyoa mithili ya mtama unaomwagika kati huku pembeni kukichongeka ni mtindo wa kijana wa Brazil mwenye kipaji, Neymar?
Inajulikana pia kwamba kunyoa na kuacha kapembetatu ni wazo lililoletwa hadharani kwa vitendo na Ronaldo wakati wa michuano ya kombe la Dunia la mwaka 1998.
Upo mtindo wa kuacha nywele nyingi za rangi ya dhahabu kichwa kizima – huu ni mtindo aliokuja nao kiungo wa Colombia, Carlos Valderrama. Kwa mitindo yao ya nywele, utawafahamu wote.
Lakini kuna zaidi ya hayo kutokana na tangazo lile. Mamadou Sakho anaposigishana wakati akipishana na Mario Balotelli na kumwambia; “tuonane dimbani”, inaeleweka wazi.
Ni bahati mbaya tu kwamba kushuka kwa kiwango cha uchezaji wa Sakho kumemfanya aondoshwe kwenye timu ya taifa, vinginevyo angekumbana na Ballotelli kwenye mechi kati ya Italia na Ufaransa.
Kisha ukaja mgogoro wa mwaka 2010, kwa timu yenye wachezaji wengi weusi kwenye fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini kuzozana hadharani na kocha wao.
Walifikia hatua ya kufanya mgomo kuonyesha mshikamano wao kwa mshambuliaji Nicolas Anelka aliyemtukana kocha Raymond Domenech. Hata hivyo, Anelka aliyekuwa amemwambia kocha wake yangekubalika miongoni mwa mashabiki wengi – hawakuweza kushinda hata mechi moja.
Anguko hilo lilisababisha mzozo wa kitaifa, huku serikali ikiagiza tume ya uchunguzi.
Miezi kadhaa baadaye, iliibuka kashfa mpya, ilipobainika kwamba kocha mpya, Laurent Blanc, alizungumzia haja ya kuweka idadi ya mwisho ya juu ya wachezaji weusi au Waraabu kwenye mafunzo ya soka kwa vijana nchini Ufaransa.
Kwa msisitizo, Blanc alikuwa akisisitiza kupata wachezaji wa “utamaduni na historia yetu”.
Bado lakini, nusu au zaidi ya nusu ya wachezaji wa kikosi cha Ufaransa kwenye Euro 2012 ni wenye asili ya kusini mwa Jangwa la Sahara na Maghreb.
Ndivyo ilivyo pia kwa Uholanzi (japokuwa asili ya makoloni ya wachezaji wao inajumuisha Indonesia na Suriname).
Takriban theluthi moja ya kikosi cha England ni wachezaji chotara, wengi wana asili ya Caribbean. Soka ya Uingereza haikupungukiwa nyakati chafu za ubaguzi kwenye hstoria yake.
Kwa mfano, mwaka 1994 gazeti la The Guardian liliripoti maelezo ya aliyekuwa kocha wa England kwamba alielekezwa na shirikisho la soka kuepuka “kuteua wachezaji wengi weusi” katika timu ya taifa.
Ujerumani ni eneo jingine barani Ulaya lenye mchanganyiko wa wachezaji wenye asili tofauti kuliko hata ilivyokuwa muongo mmoja uliopita. Kikosi chake leo hii kina sura za wachezaji ambao wazazi wao ni Wanigeria, Waturuki, Wamorocco, Wapoland na Wahispania.
Kwa muda mrefu, timu ya taifa ya Ureno imekuwa na wachezaji kadhaa wa Kibrazili (rejea akina Deco, au leo mlinzi wa Real Madrid, Pepe). Bila kumsahau mchezaji kutoka Msumbiji Eusébio da Silva Ferreira, aliyetia fora mwaka 1966 kwenye kombe la dunia na hii leo wapo akina Nani.
Sweden je? Hii ni moja ya nchi za Ulaya zilizojifungua zaidi kupokea wakimbizi. Mara nyingi imekuwa na wachezaji wa rangi tofauti, na timu yake ya sasa ina wenye asili ya Albania (mmoja wao ni mshambuliaji hatari wa Inter Milan, Zlatan Ibrahimovic) na Muiran.
Katika hali hii, wapo wachezaji wengi wenye asili ya wahamiaji watakaokuwa katika ushindani wa Euro 2012.
Denmark ina mchezaji mmoja mzaliwa wa Ivory Coast wakati Eduardo – mchezaji wa zamani wa Arsenal anayechezea timu ya taifa ya Croatia ni Mbrazili.
Timu ya taifa ya Czech inajumuisha mchezaji ambaye wazazi wake wamezaliwa nchini Ethiopia. Ugiriki nayo ina mchezaji aliyezaliwa Ujerumani, mama yake anatoka Uruguay. Wana mwingine aliyezaliwa Albania.
Kuna baadhi ya timu hazina wachezaji wahamiaji – Ukraine na Urusi (lakini zina mchezaji mwenye asili ya Tatar na mwingine kutoka Ingushetia).
Jamhuri ya Ireland na Poland zina sifa gani katika haya? Poland ilionyesha ubunifu wa aina yake na kushangaza, japo kwa uzuri, kwa mwaka 2000 kumpa uraia mshambuliaji wa Nigeria, Emmanuel Olisadebe.
Alipata uraia huo baada ya kwenda Poland kuchezea timu ya Polonia Warszawa. Baada ya kupewa uraia, aliteuliwa kwenye timu ya taifa. Hadi hivi karibuni pia, walikuwa wakimchezesha mshambuliaji wa Kibrazili, Roger Guerreiro.
Tusisahau kwamba kuna Italia. Mario Balotelli ni mchezaji wa kwanza mweusi kupeperusha bendera ya taifa kupitia Azzurri. Huyu anaonekana wazi tofauti yake.
Italia, hata hivyo haifanyi jitihada kubwa za kunasa wahamiaji mahiri wa soka kwa ajili ya Azzurri, zaidi ya Wa Argentina wenye majina yanayoonyesha asili ya Italia.
Mwingine aliye tofauti kwenye timu ya taifa ya Italia ni mlinzi Angelo Ogbonna, baba yake ni Mnigeria na mlinzi wa kati wa AC Milan, Tiago Motta kutoka Brazil.
Ubaguzi unaweza kuwapo zaidi kwenye soka ya Ukraine. Timu yao ya taifa haina wahamiaji, japokuwa ligi yao imetawaliwa na wageni. Dynamo Kiev ina Wabrazili watano, Wanigeria watatu na Mmoroco mmoja.
Shakhtar Donetsk ina wachezaji wanane kutoka Brazil (ukimhesabu Eduardo watakuwa tisa) na Mnigeria mmoja. Klabu ya Metallist Kharkiv ina Wabrazili wanne, Waargentina sita na Msenegali mmoja.
Hali hiyo inalalamikiwa na kocha wa timu ya taifa ya Ukraine, Oleg Blokhin, mchezaji mahiri wa zamani katika timu ya taifa enzi za Soviet.
Tusemeje kuhusu Hispania? Mabingwa hawa wa Ulaya wana ligi iliyojaa wachezaji wa kigeni, lakini timu yao ya taifa ni ya weupe hasa.
Lakini timu ya taifa iliyotwaa Kombe la Euro mwaka 2008 ilikuwa na mchezaji mwenye asili ya Brazil, Marcos Senna. Kikosi cha sasa kina Thiago Alcantara naye akiwa na asili ya Brazil pia.
Sakata la ubaguzi wa rangi katika soka ya Uhispania lilibainishwa kabla ya michuano ya Euro 2004. Kocha wake, Luis Aragones alinaswa kwenye runinga akimwambia mshambuliaji ‘Jose Antonio Reyes’ kua ni bora kuliko mwenzake wa Arsenal, Thierry Henry. Lakini Aragones alimtaja Henry kama “kile kinyesi cheusi.”
Uingereza imekuwa na kesi za watu maarufu kuhusu ubaguzi michezoni, na habari zao zimetawala vyombo vya habari.
Luis Suarez wa Liverpool alifungia mechi nane kwa kumshambulia kwa maneno ya kibaguzi nahodha wa Manchester United, Patrice Evra wa Ufaransa wakiwa mchezoni.
Lakini aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza na Chelsea, John Terry anakabiliwa na kesi ya kumbagua kwa rangi yake Anton Ferdinand wa Queen Park Rangers (QPR). Amenyang’anywa unahodha wa taifa kwa ajili hiyo.
Lakini kocha mpya wa England, Roy Hodgson amemrejesha kikosini Terry, jambo linaloaminika limechangia kuachwa kwa beki mahiri mweusi wa Manchester United, Rio Ferdinand, kakaye Anton. Aliwahi kusema kwamba ingemuwia vigumu kucheza na Terry.
Chama cha Wachezaji wa Kulipwa cha Uingereza kilshapitisha kuwa kosa kubwa kumbagua mchezaji kutokana na rangi yake, kosa linaloweza kukatisha mkataba wa mchezaji.
Katika zama hizi, wachezaji hawatakiwi kuhukumiwa kutokana na rangi ya ngozi, nywele au macho, bali kwa uwezo wao uwanjani.
Dimbani sasa, soka inayo mengi ya kudhihirisha Ulaya iliyoupa kisogo ubaguzi kwa mchezo safi. Nendeni kwa nguvu, Theo na Alex, Mario na Zlatan, Samir na Karim na wengineo.
Ingieni mashindanoni na muwanyamazishe manazi mamboleo wanaozitia aibu zama hizi. Wafikishieni ujumbe kwamba Ulaya hawataki kuona tena ubaguzi. Waonyesheni Ulaya wasiyotaka kuiona, lakini ambayo watakuwa bora zaidi wakiizoea.
-BBC