Wananchi kuweni wajasiri kuwataja wanaohujumu misitu.

Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki Dkt. Felician Kilahama

MKURUGENZI wa misitu na nyuki hapa nchini Dkt. Felician Kilahama,
amewataka wananchi kuwa wajasiri kuwataja viongozi wanaohusika katika
uharibifu wa misitu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao

Dkt. Kilahama aliyasema hayo Jana mkoani Kilimanjaro mara baada ya
kutembelea msitu wa Rau ulioko katika manispaa ya Moshi ambapo
alikamatwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Frank John aliyekutwa
akikata kuni ndani ya msitu huo kwa kutumia shoka na mapanga Matatu
ambayo watu walikuwa wakipita nayo katika njia zilizoko katikati ya
msitiu jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Alisema kumekuwepo na tuhuma nyingi zinazoelekezwa kwa viongozi wa
misitu na maliasili kuhusika katika uharibifu wa misitu lakini hakuna
ushahidi dhidi ya tuhuma hizo hivyo ni vema wananchi ambao
wanawafahamu viongozi wanaohiusika wakatoa ushirikiano na kuwataja ili
hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa ikiwa ni njia moja wapo ya
kukomesha vitendo hivyo ambavyo ni vya kinyume cha sheria.

“Ni kweli tumepata tuhuma nyingi dhidi ya viongozi wa misitu na
maliasili kuhusika katika uharibifu wa misitu kwa kukata miti kinyume
cha sheria na taratibu,lisemwalo lipo kama halipo laja, lakini tatizo
kubwa ni kwamba wananchi wamekuwa hawakotayari kuwataja viongozi
wanaohusika, sasa nawaomba wawe wajasiri na wawataje viongozi
wanaohusika bila woga ili wadhibitiwe kwani ni ya heri wakaacha kazi
kuliko wakaendelea kufanya vitendo vya kuhujumu misitu”alisema Dkt.
Kilaha.

Katika hatua nyingine Dkt. Kilahama aliwataka viongozi wa misitu na
maliasili hapa nchini kusimamia sheria na taratibu kikamilifu na
kuhakikisha wanawadhibiti watu wanaopita katikati ya misitu wakiwa na
zana kama mashoka,panga, misemeno na nyinginezo kwa mujibu wa sheria
kwani kuendelea kuvifumbia macho vitendo hivyo ndiko kunakotoa mwanya
wa uharibifu.

Aidha aliwataka wataalamu wa misitu na nyuki hapa nchini kuongeza
nguvu katika kudhibiti uharibifu wa mazingira na ukataji wa miti ya
asili katika misitu ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi wakati wote
wa mchana na usiku , hatua ambayo itasaidia kuunusuru misitu ambayo
kwa sasa imeonekana kuharibiwa vibaya.

“Naomba uongozi wa misitu na maliasili ukaze buti katika kudhibiti
uharibifu wa misitu,kwani wao wakilala usiku watu ndio wanafanya
kazi,wahakikishe ulinzi unakuwepo kwa saa 24 katika misitu,na kwa
kufanya hivyo watasaidia kuinusuru misitu ambayo kwa sasa imeharibiwa
sana”alisema.

Akizungumza Meneja misitu ya hifadhi mkoani Kilimanjaro Bw.Julius
Mkumbo alisema uvunaji wa miti katika misitu bado ni changamoto kubwa
lakini kwa sasa wameongeza nguvu katika mapambano ya udhibiti licha ya
kukabiliwa na tatizo kubwa la ulinzi.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Bw. Jafari Michael alisema
msitu wa Rau ulioko katika manispaa hiyo ukitunzwa vizuri utaweza
kuwa kivutio kikubwa cha utalii na chanzo cha ajira hivyo ni vema
ukatunzwa kwa ushirikiano wa ngazi zote kuanzia za mitaa hadi wizara.

Aliongeza kuwa ni vema wizara ikasimamia watumishi wake kikamilifu na
kuhakikisha wanatoka maofisini na kutembelea misitu ili kuweza kubaini
uharibifu kutokana na kwamba katika maeneo mengi watumishi wa misitu
na maliasili wamekuwa ni viongozi wa maofisini.