Basi la Sumry laua 13 kwenye ajali Mbeya

Na Ezekiel Kamanga,

Mbeya

AJALI mbaya ya basi la kampuni ya Sumry lililokuwa linatoa huduma ya usafiri kutoka Arusha kuelekea mkoani Mbeya iliyotokea eneo la Igawa mpakani mwa Mbeya na Iringa imeua watanzania 13 papo hapo na wengine watatu kufia katika hospitali ya wilaya ya Mbarali na wengine 9 kujeruhiwa miili yao.
Ajali hiyo imetokea baada ya basi hilo aina ya Nissan Dissel lenye namba za usajili T 649 BCT lilipata ajali hiyo majira ya saa nne usiku wa kuamkia leo likitokea Arusha baada ya kupasuka gurudumu lake la mbele.

Majeruhi wa ajali hiyo wamesema kuwa kabla ya ajali hiyo walisikia mlio wa gurudumu baada ya kupasuka ndipo gari ikaanza kupoteza mwelekea ambapo vaadhi yao hawakutambua kilichokuwa kikiendelea mpaka pale walipofikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali na kulazwa.

Baadhi ya Majeruhi hao walipoulizwa kuhusu mwendo kasi wa gari hiyo kabla halijapinduka walisema kuwa hawajui kama dereva wao alikuwa kwenye mwendo kasi bali wanachokijua ni kwamba ajali hiyo imetokea kutokana na kupasuka gurudumu lake.Mwandishi wa habari hizi alipofika katika  hospitali ya wilaya ya Mbarali na hatimaye kufika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kushuhudia miili ya marehemu waliofariki katika ajali hiyo ikiwa katika  chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya wazazi Meta iliyopo chini ya Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Baada ya nyendo hizo na kujua undani wa tukio hilo na baadhi ya majina ya majeruhi na marehemu, kipindi hiki kimepiga hodi ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi na kupata ushirikiano kutoka ofisi ya Mkuu wa kitengo cha Upelelezi mkoa wa Mbeya.

Katika ajali hiyo waliopoteza maisha na baadhi kutambuliwa majina kufikia majira ya saa tisa alasiri ni pamoja na dereva wa basi hilo Makame Juma(54), Frolencia Kitaule, Thomas Ncharo, Martha Mgeta na Bupe Mwaijumba ambaye ni askari polisi mkoani Kilimanjaro.

Majeruhi walionusurika katika ajali hiyo na kuendelea kutukuza utukufu na ukuu wa Mungu wao ni Rajab Fikiri, Rupi Mwaipalo, Martin Costantino, Tadei Msangi, Endrew Ndalepa, Ezekiel Ndalepa, Riziki Chuwa, Erasto Kiwanga, Salehe Mohamed, Bakari Zayumba, Halima Abdallah na mtoto mmoja mdogo mwenye jinsia ya kike ambaye hajaweza kujieleza wala kusema wazazi wake wako wapi (huenda wamefariki).Ajali hiyo imethibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa huku likisema utambuzi zaidi wa watanzania waliopoteza maisha yao ukiendelea kufanyika.