Maharamia kushtakiwa Mauritious

UINGEREZA imetia saini mkataba na Mauritious kuruhusu washukiwa wa uharamia waliokamatwa na jeshi na wanamaji kupelekwa kisiwani humo kwa mashtaka.
Waziri mkuu David Cameron alikutana na mwenzake wa Mauritious Navin Ramgoolam nchini Uingereza kwa makubaliano hayo.
Cameron ameutaja mkataba huo kama hatua muhimu katika vita dhidi ya maharamia sugu wanaoendesha harakati zao katika upembe wa Afrika.
Makubaliano sawa na hayo kati ya nchi hiyo na Tanzania yaliafikiwa katika siku za nyuma.
“Hii ni muhimu sana , mojawapo ya hatua za kufuatilizia mkutano wa London na Istanbul kuhusu Somalia mwaka huu na ni dalili kuwa nchi zingine katika ufuo wa bahari Hindi zinafanya juhudi kubwa dhidi ya uharamia,” alisema bwana Cameron.
“uharamia ni kitndo cha uhalifu, na maharamia wanapaswa kufahamu kuwa watakamatwa wakiendesha shughuli zao hata baharini, washtakiwe na kufungwa jela.”
Jeshi la wanamaji la Uingereza na majeshi mengine kote duniani yanashika doria katika sehemu ambazo zina shughuli nyingi za meli na ambapo kuna tisho la uharamia.
Mabaharia hukamatwa na kuachiliwa tu wakati kikombozi kikitolewa, na kuwekwa katika mazingira mabaya huku baadhi wakiteswa ili kushinikiza wamiliki wa meli zao kutoa kikombozi.
Uharamia katika pwani ya Somalia, unaaminika kugharimu makampuni ya meli za mizigo takriban dola bilioni 5.6 mwaka jana pekee.

-BBC