Yono Stanley Kevela kuwania uongozi Yanga

Yono Stanley Kevela

“NDUGU wanahabari na mashabiki wa soka, napenda kuwajulisha kuwa nimechukua fomu mbili za kuwania uongozi ndani ya Klabu yetu ya Yanga, moja ni ya kuwania Makamu Mwenyekiti na nyingine ikiwa ni kuwania nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji,” anasema Kevela katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

“Nimelazimika kuchukua fomu za nafasi hizo mbili ili kuwaachia wanachama wa Yanga kunipima na kuona ni katika nafasi ipi wanaona naweza kuwatumikia ipasavyo ili kuiletea Klabu yetu mafanikio zaidi kuliko ilivyo sasa.”

“Nina uzoefu mkubwa katika uongozi kwa tasnia zote kuanzia michezo, siasa, biashara na masuala mengine yanayoizunguka jamii. Uzoefu katika michezo unatokana na ushiriki wangu katika masuala kadhaa yanayoihusu Yanga yenyewe na michezo mingine kadhaa.” anaeleza Kevela.

Alisema ushiriki wake kwa Yanga amekuwa akiutoa kwa uongozi wa Yanga kwa vipindi tofauti kunishirikisha katika baadhi ya masuala yanayoihusu Klabu.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ndiyo iliyowezesha uongozi wa Yanga mwaka jana kumteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Ushindi hatua iliyoiwezesha Timu kutwaa Ubingwa wa Bara. Alieleza kuwa amekuwa akisaidia wachezaji wa zamani wa Yanga (Yanga Veterans) kushiriki katika michezo mbalimbali ili kuendelea kuimarisha afya zao baada ya kustaafu soka.

Aliongeza kuwa kisiasa amewahi kuwa Mbunge wa Njombe Magharibi, nafasi ambayo iliniwezesha kuzisaidia timu kadhaa za michezo ikiwemo Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake (Twiga Stars) na Yanga yenyewe.Katika hatua nyingine ya kuthamini michezo kupitia nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kampuni ya Yono Auction Mart nilianzisha timu ya Soka ya Yono ambayo imekuwa ikishiriki katika michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi, sababu zinazothibitisha kwamba nimekuwa jirani na soka kwa muda mrefu sasa.

LENGO KUU

Nimeshawishika kuwania uongozi ndani ya Yanga nikiwa na Kauli Mbiu ya ‘Maslahi ya Wachezaji Kwanza’, kauli mbiu yenye lengo la kuboresha maslahi kwa wachezaji wa Yanga ili kuinua kiwango cha soka letu na hivyo kutamba katika michezo ya ndani na nje ya nchi.

Nikichaguliwa kuingia katika uongozi wa Yanga nitashirikiana na viongozi wenzangu katika kuvunja makundi ili kuwezesha kuwa na Yanga Moja Imara itakayotuvusha kutoka katika soka la sasa lisilo na tija hadi katika soka la kisasa lenye mafanikio kwa Klabu, Wachezaji na Wanachama wote.

Nimejitupa katika kuwania uongozi ndani ya Yanga bila kuwa na ajenda ya siri. Baadhi ya wanaYanga wamekuwa wakijitokeza kuwania uongozi wakiwa na ajenda za kutaka kujinufaisha wao binafsi badala ya klabu na wachezaji.

Yanga inaweza kuwa Timu Bora na Imara tofauti na sasa kama itapata viongozi watakaoimarisha matawi ya Klabu ambayo mengi yanasuasua na pia atakayeweza kubuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vile vilivyopo kama majengo na vinginevyo kwa kuthubutu na kujiamini, sifa ambazo mimi ninazo.

Naamini kwa pamoja tutajenga Yanga Bora na Yanga Imara.
YONO STANLEY KEVELA