Sweden yaahidi ushirikiano Zanzibar

SWEDEN imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo pamoja na kuwa balozi wa kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata katika sekta hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Tanzania . Lennarth Hjelmaker, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha na kufanya mazungumzo na Rais.
Katika maelezo yake Balozi Hjelmaker alisema kuwa Sweden inajivunia uhusiano na mashirikiano makubwa yaliopo kati yake na Tanzania, ikiwemo Zanzibar na kuahidi kuendeleza ushirikiano na uhusiano wake wa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo elimu, nishati na nyenginezo.
Balozi Hjelmaker alisema kuwa Sweden inatambua mafanikio yaliofikiwa katika uimarishaji wa sekta ya utalii hapa Zanzibar sanjari na vivutio vyake viliopo hapa nchini na kueleza kuitaiganza Zanzibar nchini kwake ili wananchi wa nchi yake waendelee kuitebelea Zanzibar.
Mbali ya kuelezea juu ya sekta ya utalii na mafanikio yaliofikiwa pamoja na lengo lake la kuwahamasisha wananchi wa Sweden kuja kuitembelea Zanzibar, Balozi huyo alitoa pongezi kwa Zanzibar kwa kuendeleza Utawala Bora na kulinda na kuendeleza haki za wananwake na watoto.
Aidha, balozi huyo aligusia jitihada mbali mbali zinazoendelezwa na Serikali yake pamoja na Jumuiya zisizo za Kiserikali (NGOs), katika kukuza mashirikiano na kuimarisha maendeleo hapa nchini.
Katika mazungumzo yake balozi huyo alieleza jinsi walivyofurahia sherehe za siku ya uhuru wan chi yake zilizofanyika huko Dar-es-Salaam hapo jana kwa upande wa Tanzania na kueleza kuwa katika hotuba yake alisisitiza azma ya nchi yake ya kuendeleza ushirikiano na Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Pamoja na hayo Balozi huyo alifurahishwa na juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha amani na utulivu na kuendelea kuahidi kuwa nchi yake pia, itashirikiana na Zanzibar katika sekta ya biashara na utalii.
Nae Dk. Shein alisema kuwa Sweden imekuwa na mashirikiano ya muda mrefu na Sweden hatua ambayo imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa nchi hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo hasa katika sekta ya elimu kwa kupitia Shirika lake la SIDA, nishati na sekta nyenginezo.
Kwa upande wa sekta ya Utalii, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya kuufanya utalii kuwa sekta mama kutokana na mchango wake mkubwa wa pato la taifa kutokana na vivutio kadhaa vilivyopo ambavyo vimekuwa vikiwavutia wageni kutoka ncghi mbali mbali ikiwemo Sweden na kumuhakikishia Balozi huyo amani na utulivu nchini.
Aidha, Dk. Shein aliipongeza Sweden kwa kuunga mkono jitihada za Zanzibar za kuimarisha Utawala Bora na imekuwa na historia kubwa katika uanzishwaji wa harakati za Utawala Bora hapa nchini.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali katika kutafuta vyanzo vyengine vya nishati ambapo tafiti mbali mbali zimekuwa zikifanywa ili kutafuta vyanzo hivyo mbadala hasa katika nishati zinazorejesheka ikiwemo mawimbi ya baharim jua upepo na takataka.
Dk. Shein aliipongeza Sweden kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala ya wanawake na watoto kupitia Serikali Kuu na Mashirika yake ambapo pia aliishukuru kwa ushiriki wake katika kuunga mkono juhudi za serikali katika uhifadhi wa mazingira.
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Mhe. Amour Zacaria aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumuaga Rais.
Katika mazungumzo hayo Dk Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta ya miundombinu hasa katika ujenzi wa barabara kuu, ambapo hadi kufikia mwa ka 2013 matarajio makubwa ya kuwa barabara zote kuu zitakuwa zimefikia katika ujenzi wa kiwango cha lami.
Alisema kuwa maendeleo makubwa yaweza kupatikanwa katika kuimarisha sekta ya elimu, afya, Utawala Bora, Kilimo, Utalii na sekta nyenginezo na kumueleza balozi huyo haja ya kushirikiana katika sekta ya biashara kati ya Msumbiji na Zanzibar.
Nae Balozi Zacaria alimueleza Dk. Shein kkuwa nchi yake imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha uchumi wake ambao hivi sasa umekuwa kwa asilimi tisa na kumueleza juhudi zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, njia za reli na bandari ambazo zitaimarisha pia, sekta ya ajira nchinin humo.
Aidha, alielezajitihada mbali mbali zinazochukuliwa na chi yake katika uchunguzi na utafiti katika uchimaji wa gesi pamoja na makaa yam awe kama ni njia moja wapo ya kuongeza vyanzo vya nishati ambapo hivi sasa tayari nchi hiyo inazalisha tani milioni 2 kwa mwaka. Pia alimueleza Rais kuwa ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kuimarisha nishati unaendelea.
Pamoja na hayo, Balozi huyo alieleza kuwa licha ya mafanikio yaliopatikana katika sekta nyenginezo lakini kilimo bado kinabaki kuwa ni sekta muhimu kwa nchi hiyo ya Msumbiji ambapo hivi sasa serikali imeteua mikoa mitatu kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo cha biashara ambapo hayo yote yanalenga kupunguza utegemeaji wa chakula kutoka nje.
Balozi huyo, alieleza kuwa hali ya nchi hiyo ni ya usalama na inaendelea vizuri na kumueleza kuwa nchi hiyo inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu mwaka 2014 na kumueleza mafanikio yalioppatikana na chama cha FRELIMO katika kuongoza dola.