RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametoa maagizo thabiti saba ya kuhifadhi mazingira nchini akisema “tusipokuwa makini na kuchukua hatua thabiti za kuhifadhi mazingira, uhai na ustawi wetu utakuwa mashakani. Tusipofanya hivyo, huko mbele ya safari kuna giza nene la maangamizi.”
Aidha, Rais Kikwete ametoa mifano saba ya kuthibitisha uharibifu wa mazingira duniani na kueleza njia nne ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia katika uharibifu wa mazingira nchini.
Amesisitiza kuwa jukumu la kutunza na la kuhifadhi mazingira ni la Watanzania wote, linalohitaji juhudi za pamoja na ushirikiano wa karibu wa wadau wote katika ngazi zote nchini.
Rais Kikwete ameeleza athari hizo za mazingira na hatua za kuchukuliwa kupambana na hali hiyo wakati alipohutubia mamia ya wananchi kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi kwenye Kilele cha Maadhiminisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambako pia amezindua Kampeni ya Kitaifa ya Usafi na Ujenzi wa Vyoo Bora.
Baada ya kueleza kwa ufasaha kuhusu athari za uharibifu wa mazingira nchini, Rais Kikwete ametoa maagizo thabiti saba ya jinsi ya kupambana na hali hiyo nchini ikiwa ni pamoja na kuzingatia umuhimu wa kuhifadhi ardhi na misitu kwa kupanda miti; kuhifadhi vyanzo vya maji, milima na misitu ya asili; na kudhibiti kilimo, ufugaji na uchimbaji wa madini usiokuwa endelevu.
Maagizo mengine ya Rais Kikwete ni kudhibiti matumizi mabaya ya dawa za mifugo na kilimo; kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya makazi na viwandani; kusimamia uzalishaji bora usiochafua mazingira kwenye viwanda nchini; na kulinda mazingira ya pwani, mito, maziwa na bahari.
Rais Kikwete pia amewaeleza wananchi mifano saba ya kuthibitisha jinsi hali ya mazingira ilivyoharibika duniani ikiwa ni pamoja na ukweli kuwa majira ya mvua yamebadilika, mvua siyo ya uhakika na vipindi vya ukame vimeongezeka; theluji inapungua kwa kasi kwenye ncha za Kaskazini na Kusini mwa dunia na kwenye vilele ya milima ukiwamo Mlima Kilimanjaro; na kuongezeka kwa maji baharini na hivyo kuzidi kula nchi kavu na kuyaweka maeneo mengine katika hatari ya kumezwa na maji.
Mifano mingine ni magonjwa kama malaria kuzidi kusambaa katika maeneo ambayo zamani yalikuwa hayana mbu kwa sababu yalikuwa baridi na sasa yamekuwa joto; kuzidi kupungua kwa maji safi kwenye mito, chemichemi, vijito, maziwa na mabwawa; kuzidi kuendelea kupungua kwa eneo la misitu na kusambaa zaidi kwa jangwa; na kupungua kwa ubora wa ardhi na hivyo kupungua kwa mazao na malisho ya mifugo.
Kuhusu uharibifu wa mazigira nchini, Rais Kikwete amesema kuwa umekuwa unachangiwa pamoja na mambo mengine ukataji miti kwa wingi kwa ajili ya shughuli za kilimo; uvunaji miti kwa kasi zaidi kuliko ile inayopangwa; kuwepo kwa mifugo mingi kupita uwezo wa ardhi; na shughuli za viwanda na hasa mahitaji ya nishati na malighafi kusababisha uharibifu wa mazingira.
Kuhusu umuhimu wa kushirikiana kupambana na janga la uharibifu wa mazingira, Rais Kikwete amewaambia wananchi: “ Jukumu la kutunza na kuhifadhi mazingira ni letu sote, linahitaji juhudi za pamoja na ushirikiano wa karibu wa wadau husika katika ngazi zote. Sisi peke yetu Serikalini hatuwezi kwani wahenga wamesema: ‘kidole kimoja hakivunji chawa.’ Tunataka wote tuhusike – Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, wananchi, NGO’s na kadhalika.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda kutumia nafasi hii kuzipongeza baadhi ya Serikali za Mitaa ambazo zimeunda Kamati za Mazingira ili kuratibu shughuli za kuhifadhi mazingira katika maeneo yao. Napenda kutoa mwito kwa Serikali za Mitaa ambazo bado hazijaunda Kamati hizo, wafanye hivyo mapema iwezekanavyo. Tayari nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kusimamia kwa makini Sheria na Kanuni za Hifadhi ya Mazingira katika maeneo yao. Natumaini hili litafanyika.”
Wakati wa sherehe hizo, Rais Kikwete pia amewakabidhi washindi wa mwaka huu wa mashindano ya usafi nchini na washindi wa mashindano ya kuhifadhi mazingira nchini ambako Shule ya Sekondari ya Kameyu ya Mkoa wa Manyara imechukua ushindi wa jumla wa ubora wa kuhifadhi na kutunza mazingira nchini.
Aidha, wakati wa sherehe hizo, Rais Kikwete amezindua Kampeni ya Taifa ya Usafi na Ujenzi wa Vyoo Bora ambao unaendeshwa kwa ushirikiano baina ya Serikali, Wananchi na Washirika wa Maendeleo wa Tanzania ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Watoto (UNICEF).
Mapema leo asubuhi, Rais Kikwete amezindua Mpango wa Upandaji Miti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini ambako maelfu kwa maelfu ya miti itapandwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Rais amezindua Mpango huo kwa kupand mti aina ya Mzeituni kwenye eneo la Hosteli ya Uhuru mjini Moshi.