Mahakama yaamuru Mbowe, Dk Slaa, Ndesamburo wakamatwe

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe

Na Janeth Mushi
Arusha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha imetoa amri ya kukamatwa kwa watuhumiwa nane (8) pamoja na wadhamini wao, wakiwemo Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Freeman Mbowe na Dk. Willbrod Slaa kisha kufikishwa mahakamani hapo wakati wowote.

Viongozi wengine ambao nao wanatakiwa kukamatwa ni Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Philemon Ndessamburo pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa alitoa hati ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao pamoja na wadhamini wao kutokana na wao pamoja na wadhamini wao kutofika mahakamani bila taarifa ilhali wakijua wanatakiwa kuhudhuria kesi yao.

Aidha alisema watuhumiwa wengine wanaotakiwa kukamatwa ni mke wa Dk. Slaa, Josephine Mshumbusi, Aquiline Chuwa pamoja na Richard Mtui ambao hawakufika pia mahakamani hapo wala wadhamini waliokuwa wamewadhamini.

Kesi hiyo ambayo ilikwama kusikilizwa maelezo ya awali katika mahakama hiyo Aprili 29 mwaka huu kutokana na baadhi ya watuhumiwa kushindwa kufika mahakamani, akiwemo mke wa Dk. Willbrod Slaa, Mshumbusi aliyedaiwa kuwa ni mgonjwa, Mathias Valerian na Dadi Igogo ambao nao walidaiwa wagonjwa na hivyo shauri hilo kutoanza kusikilizwa.

Akifafanua zaidi Hakimu alisisitiza juu ya uwepo wa watuhumiwa wote katika usikilizwaji wa awali wa shauri hilo kutokana na ulazima wa mtuhumiwa kuwepo mahakamani ili kutamka iwapo anakubali ama anakataa mashitaka yanayomkabili na kuweza kusaini hati ya maelezo.

Hata hivyo, kabla ya Hakimu huyo kuahirisha kesi hiyo Aprili 29 aliwakumbusha watuhumiwa hao kuzingatia masharti ya dhamana waliyopewa ikiwa ni pamoja na kufika mahakamani pindi shauri lao linapotajwa na kuwaonya kuwa ambao hawatazingatia pasipo sababu mahakama itawafutia dhamana.

Pamoja na hayo Magesa alisema dhamana kwa watuhumiwa ambao walifika mahakamani na wale waliowakilishwa na wadhamini wao bado zinaendelea na kuwataja kuwa ni Basil Lema, Nai Steven, John Materu, Peter Marua, Mathias Valerian, Walter Mushi na Juma Samweli.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa

Wengine ni Daniel Titus, Derick Magoma, kwa upande wakw Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alitolewa udhuru na mdhamini wake kuwa yuko Bagamoyo katika vikao vya Kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Dadi Igogo ilidaiwa kuwa yuko katika Mitihani.

Aidha katika kesi hiyo mawakili wa upande wa utetezi hawakuweza kufika mahakamani hapo, wala taarifa zao hazikuweza kufika ambao ni Method Kimomogolo na Albert Msando.

Mahakama hiyo iliahirisha shauri hilo na inatarajia kuanza kusikiliza hoja za awali hapo Juni 24, 2011 baada ya wakili wa upande wa Serikali, Edwin Kakolaki kuiomba mahakama kuanza kusikiliza shauri hilo.