Na mwandishi wetu Kilimanjaro
SERIKALI imekiri kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa Mazingira
unaosababishwa na shughuli za binadamu,na kusema kuwa hali kwa sasa ni
mbaya na watu wasipokuwa makini na kuchukua hatua za makusudi za
kuhifadhi mazingira uhai na ustawi wa nchi utakuwa mashakani.
Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
aliyasema hayo jana mjini Moshi wakati akifunga wiki ya mazingira
iliyokuwa ikiadhimishwa kitaifa mkoani Kilimanjaro kuanzia Juni Mosi
ikiwa na kauli mbiu isemayo hifadhi mazingira jikite kwenye uzalishaji
endelevu na kuzindua kampeni ya usafi kitaifa inayoanza mwaka huu.
Dkt. Kikwete alisema ni ukweli uliowazi kwamba mazingira yameharibiwa
vibaya na bado tunaendelea kuyaharibu,hali ambayo imesababisha
madhara makubwa ikiwa ni pamoja na nchi kuingia gizani kutokana na
ukame wa muda mrefu uliotokana na kubadilika kwa majira na mvua
szisizotabirika.
Alisema tusipokuwa makini katika suala la mazaingira na kuchukua hatua
za dhati za kuhifadhi mazingira,huko mbele ya safari kuna giza nene la
maangamizi ambalo litafanya watu wafe na uwe mwisho wa dunia.
“Huu mchezo wa uharibifu wa mazingira tunaoufanya sasa,utafanya tufe
na iwe mwisho wa dunia,kwani ni ukweli uliowazi kuwa tumefanya na
tunaendelea kufanya uharibifu wa mazingira na hivi sasa tayari
tunaonja na kuteswa na athari za uharibifu wa mazingira
tuliofanya”alisema Dkt.Kikwete.
Alisema madhara mengine yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira ni
kupungua kwa kasi kwa theluji katika vilele vya milima duniani
ikiwemo mlima wa Kilimanjaro,kuongezeka kwa maji baharini na kula
maeneo ya nchi kavu hali iliyosababisha maeneo mengi kuzama na mengine
yako hatarini kuzama.
“Kwa ujumla hali si nzuri hata kidigo,hatuna budi kuchukua hatua za
dhati za kurekebisha mambo,lazima tupunguze kasi ya kuharibu
mazingira na tuendeleze juhudi za kujenga upya tulikoharibu na kulinda
palipo salama kwani matendo yetu wanadamu katika kutafuta riziki na
kujiletea maendeleo ndizo zinzosababisha uharibifu huu”aliosema.
Alisema kwa sasa hali hii haiwezi kuachwa ikaendelea,hivyo ni jukumu
la kila mwananchi kudhibiti tatizo la uharibifu wa mazingira na
kurekebisha palipoharibiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ardhi
inahifadhiwa,miti inapandwa, vyanzo vya maji vinahifadhiwa pamoja na
kudhibiti kilimo,ufugaji na uchimbaji wa madini usioendelevu.
Akizungumza Naibu waziri wa wizara ya afya na ustawi wa jamii Dkt.
Seif Rashidi alisema hali ya usafi na mazingira katika nchi bado si
nzuri na kwamba pamoja na jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na
serikali wananchi wengi bado hawajaona umuhimu wa kutumia vyoo na kuwa
na tabia ya kunawa mikono mara baada ya kutoka chooni.
Dkt. Rashidi alisema Asilimia 22 mijini na asilimia Tisa vijiniji
ndizo zinazotumia vyoo bora na watu wanne kati ya 10 ndio wanaonawa
mikono mara baada ya kutoka chooni na kwamba ili kuondokana na tatizo
hilo serikali imezindua kampeni ya miaka mnne ya usafi ambayo inaanza
mwaka huu .
Naye mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama alisema katika
kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira mkoa Kilimanjaro
umepanga kupanda miti Mil. 8.259 lakini kutokana na mkoa huo
kukabiliwa na tatizo la ukame na upungufu wa miche ya miti hadi sasa
wamepanda miti Mil. 5.604 .
Dkt. Kikwete Kabla ya kufunga wiki ya mazingira alipanda mti katika
bustani ya Miti ya kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi
ya kaskazini ambapo alilipongeza sana kanisa hilo kwa jitihada
walizonazo katika kutunza na kuhifadhi mazingira.
Awali akisoma Risala Katibu mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Julius
Mosi alisema toka kuanza kwa kampeni ya upandaji miti dayosisi hiyo
imefanikiwa kupanda miti zaidi ya Mil.1.7 na kwamba bado wanatarajia
kupanda miti zaidi ya Laki moja mwaka huu katika maeneo mbalimbali
ambapo itapandwa na wanafunzi wa Kipa imara kwabla ya kubarikiwa.
Rais Kikwete pia aligawa zawadi na tuzo kwa Halmashauri za
majiji,manispaa,miji na wilaya zilizoongoza kwenye usafi ambapo Jiji
lililoongoza kwa usafi mwaka huu ni Mwanza, kwa manispaa ni manispaa
ya Moshi,mji unaoongoza ni mpanda na halmashauri ya wilaya ni Meru.