WAKUU wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambao wamemaliza kikao chao cha siku moja na wamekubaliana kwa pamoja kwamba Serikali ya Zimbabwe haina budi kukamilisha utaratibu wa kuanzisha mchakato wa Katiba.
Uamuzi huo umefikiwa jana usiku (Ijumaa, Juni Mosi, 2012) mara baada ya Wakuu wa nchi saba za SADC na wawakilishi wa nchi saba kuhitimisha kikao cha siku moja kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Talatona (CCTA), jijini Luanda, Angola.
Katika taarifa yao ya pamoja (joint communiqué), wakuu hao wameitaka Serikali ya Zimbabwe kukamilisha mchakato wa Katiba na kisha kuitisha kura ya maoni kama ambavyo ilikubaliwa kwenye Global Political Agreement (GPA) ya SADC.
“Kikao hiki kinawataka wajumbe wa GPA wakisaidiwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye pia ni mratibu wa upatikanaji wa muafaka wa kisiasa Zimbabwe (Zimbabwe Political Dialogue) waweke mkakati wa utekelezaji wa makubaliano ya GPA utakaoainisha muda wa utekelezaji wa makubaliano hayo kuelekea uchaguzi mkuu,” ilisema sehemu ya taarifa yao.
Kikao hicho pia kiliridhia kupitishwa kwa jina la Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini, Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma kuwa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU). Mapema mwaka huu, uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo inayoshikiliwa na Bw. Jean Ping ulishindwa kufanyika kwa sababu kadhaa.
“Kikao hiki kinaipongeza Seriklai ya Malawi kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika ambao umepangwa kufanyika Lilongwe, Julai, mwaka huu. Kwa hiyo basi, kikao hiki kinataka uchaguzi wa wajumbe wa Kamisheni ya AU ufanyike wakati wa mkutano huo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na hali za kisiasa katika nchi za Congo (DRC), Madagascar na Malawi.
Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa SADC, Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuweka juhudi za makusudi katika kuimarisha miundombinu kwenye kanda hiyo ya kusini mwa Afrika.
“Tunapaswa kushirikiana kuimarisha miundombinu kwenye kanda yetu ya SADC, tukifanikiwa katika hili tutakuwa tumeweka msingi mkuu wa utangamano wa kikanda, tutaweza kusumuma ajenda ya kuleta maendeleo na kupunguza umaskini miongoni mwa nchi wanachama,” alisema.
Wakuu wengine wa nchi wanachama waliohudhuria kikao hicho ni Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama, Rais wa Botswana, Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Mfalme Mswati wa Tatu wa Swaziland, Rais Michael Sata wa Zambia na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Nchi zilizotuma wawakilishi wakiwemo mawaziri wakuu na mawaziri wa mambo ya nje ni Tanzania, Congo (DRC), Malawi, Mauritius, Msumbiji, Seychelles na Lesotho.
Waziri Mkuu ambaye alihudhuria kikao hicho kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, ameondoka Luanda, Angola leo asubuhi (Jumamosi, Juni 2, 2012) kurejea nchini.