Na mwandishi wetu
SERIKALI imewataka wafugaji hapa nchini kubadilika na kupunguza idadi ya mifugo hatua ambayo itasaidia kuondoa tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji ambalo limekuwa likiyakumba maeneo mengi na kusababisha madhara makubwa kwa binadamu ikiwa ni pamoja na vifo.
Rai hiyo imetelewa jana mjini Moshi na waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi Dkt Mathayo David wakati akifungua mkutano wa baraza la mwaka la wadau wa sekta ndogo ya maziwa ambapo alisema kumekuwepo na idadi kubwa ya mifugo ikilinganishwa na ukubwa wa maeneo hali ambayo imekuwa ikisababisha kuibuka kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji na kuvuruga amani.
Dkt. Matayo alisema ni lazima wafugaji kwa sasa wakabadilika na kuondokana na ufugaji uliopitwa na wakati wa kufuga mifugo mingi isiyo na tija na badala yake waanze kufuga kitaalamu hatua ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi.
Dkt. Matayo akitolea mfano mgogoro wa hivi karibuni uliotokea wilayani rufiji alisema mgogori huo ulitokana na mifugo kuwa mingi ikilinganishwa na ukubwa wa eneo hivyo ni vema wafugaji wakapunguza idadi ya mifugo.
“Nadhani wote mlisikia mgogoro uliotokea eneo la Ikwiriri hivi karibuni,kilichotokea pale ni kwamba katika eneo lile mifugo imeingia mingi na eneo lile ni dogo,na cha kufanya sasa ili kukabiliana na matatizo hayo ni lazima watu wapunguize mifugo na hili serikali tutalifuatilia kwa k,aribu ili kuhakikisha linatekelezeka kwa haraka”alisema Dkt. Matayo.
Aidha alisema suala la upunguzaji mifugo likishaanikiwa serikali itaanza mchakato wa kugawanya maeneo ya wakulima na wafugaji kutokana na kwamba kwa sasa zoezi hilo haliwezi kutekelezwa wakati mifugo bado ni mingi.
“Unakuta mtu ana Ng’ombe 300 halafu anaendelea kuwakumbatia pasipo faida yoyote,punguzeno Ng’ombe hao kwa faida wakati wananguvu ili muanzishe miradi mingine ya kim aendeleo badala ya kuwakumbatia na baadae kufa pasipo kuwasaidia, sasa fugeni kwa tija kuzuia uvunjifu wa amani”alisema.
Katika hatua nyingine Dkt. Matayo aliwataka wazalishaji wa maziwa hapa nchini kuacha tabia ya kuchanganya maji kwenye maziwa kutokana na kwamba tabia huyo husababisha watu kuyachukia maziwa na hivyo nchi ya Tanzania kuendelea kuwa chini katika unywaji wa maziwa.
Dkt Matayo alisema Takwimu za unywaji wa maziwa hadi sasa hapa nchini ni wastani wa Lita 44 kwa mtu mmoja kwa mwaka wakati shirika la Afya duniani (WHO) na shirika la chakula duniani (FAO) limependekeza unywaji wa maziwa ufikie angalau Lita 200 kwa mtu kwa mwaka.
“Tanzania bado hatujaweza kufikia Kiwango cha kimataifa cha unywaji wa maziwa nah iii ni kutokana na baadhi ya wazalishaji wa maziwa kuchanganya maziwa na maji,hivyo kusababisha watu kuyachukia maziwa, naomba wabadilike na waache tabia hiyo ili tuweze kupiga hatua katika unywaji wa maziwa na kufikia viwango vya kimataifa”alisema.
Hata hivyo aliwataka wadau wa maziwa hapa nchini kujipanga vizuri katika sekta hiyo na kuzalisha bidhaa zenye ubora unaohitajika katika soko la jumuiya ya Afrika mashariki ili ziweze kuhimili ushindani na bidhaa za nchi wanachama wa jumuiya hiyo kutokana na kwamba kwa sasa nchi imeshaanza ushirikiano wa kibiashara na nchi hizo.
Nao baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro waliishauri serikali kuangalia uwezekano wa kutoa uhamasishaji zaidi juu ya mazao yatokanayo na maziwa ili kufanikisha jitihada za kuinua sekta hiyo hapa nchini.
Wiki ya maziwa ambayo huadhimishwa kila mwaka kuanzia May 29 hadi jun mosi kwa mwaka huu inaadhimishiwa mkoani Kilimanjaro ikiwa na kauli mbiu isemayo, ‘kuza uchumi na Lishe,Fanya maziwa kuwa moja kati ya mazao makuu ya wilaya.