Na mwandishi wetu
HIFADHI ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) imewataka waongoza watalii katika hifadhi hiyo kufanya kazi kitaaluma hatua ambayo itawawezesha kuingia katika ushindani wa kitaifa na kimataifa na kwamba haitokubali kuendelea kuyafumbia macho makosa yasiyo ya lazima ambayo yamekuwa yakifanywa na waongoza watalii huku wageni wakiendelea kupata huduma duni.
Rai hiyo ilitolewa na mhifadhi mkuu wa Kinapa Bw.Erastus Lufungulo, wakati akifungua mafunzo ya waongoza watalii hifadhi ya taifa Kilimanjaro yanayotolewa na hifadhi hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo ambapo alisema shughuli nyingi za utalii kwa sasa zinafanywa Kisayansi na Kiteknolojia hivyo ni vema nao wakaeendelea kujiendeleza zaidi kielimu ili kujikita kwenye kilele cha utoaji huduma bora kwa watalii.
Alisema kwa sasa katika sekta ya utalii kuna ushindani mkubwa ambao ni wa kimataifa hivyo ni vema vijana wanaofanya kazi ya kuongpoza watalii wakahakikisha hawaridhiki na elimu walioipata na badala yake wajidhatiti kwa kujifunza mambo mengi yanayohusu utalii.
“Ndugu vijana waongoza watalii napenda kuwakumbusha kuwa sasa hivi sekta hii ya utalii inaushindani mkubwa,lakni pia msisahau kuwa sasa hivi watu wengi wanafanya shughuli zao Ki-sayansi na teknolojia zaidi,hivyo basi na ninyi inawalazimu kulandana nao,na ikibidi kuwazidi,ili kuendelea kuinua sekta ya utalii hapa nchini”alisema Bw. Lufungulo.
Alisema waongoza watalii ni watu muhimu sana katika sekta ya utalii kutokana na kwamba hukaa na wageni ambao ni watalii kwa saa 24 hivyo wanapaswa kupambana kiume ili kuonekana chachu katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini na duniani kote.
Aidha alisema waongoza watalii wanapaswa kuelewa mambo ya lazima yanayotakiwa kufuatwa ikiwa ni pamoja na sheria, kanuni na taratibu za hifadhi ili kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima .
“Ndugu zangu,naomba mfahamu kuwa suala hili la mafunzo si la mzaha au dogo kama wengine wanavyodhani, kwani kosa dogo katika hili linaweza kusababisha madhara makubwa kwa wageni wetu na hatimaye kutuletea lawama nyingi zitakazoweza kuharibu sifa nzuri ya utalii tuliyonayo hapa nchini”alisema.
Wakizungumza baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliishukuru hifadhi hiyo, kwa kuwapa mafunzo na kusema kuwa yatawapa uelewa zaidi wa utalii na namna ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa zilizopo katika hifadhi.
Washiriki hao waliwataka piwa wanawake kujitokeza kufanya kazi ya uongoza watalii kutokana na kwamba kumekuwepo na mtazamo potofu kuwa kazi hiyo ni ya wanaume pekee jamnbo ambalo si sahihi na kwamba limekuwa likisababisha wageni wa jinsia ya kike kukosa uhuru pindi wanapofika katika hifadhi hiyo kutokana na kukosekana kwa watalii wa kike ambao wataweza kuwa wazi kwao kuwaelezea matatizo yao.
Mafunzo hayo ambayo yanatolewa kwa waongoza watalii 1,200 yatakuwa ya nadharia na vitendo (kupanda mlima Kilimanjaro hadi Kileleni) na baada ya mafunzo hayo watapewa mtihani na watakao faulu ndio watakaopewa vitambulisho vya kuongoza watalii katika hifadhi hiyo.