Mwaka wa kimataifa wa Kemia

Na Maulid Kapolo

WAZIRI wa mawasiliano, sayansi na teknolojia Profesa Makame Mbarawa amewataka walimu, wazazi pamoja na jamii kwa ujumla kuwahamasisha na kuwashawishi wanafunzi kuanzia ngazi ya chini kupenda masomo ya sayansi hususani kemia.

Taarifa hiyo ilitolewa jana, Dar es Salaam na Profesa Mbarawa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya masomo ya sayansi nchini katika uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa kemia.

Mbarawa alisema kuwa japokuwa shule nyingi hazina maabara na vifaa vya kufanyia majaribio katika masomo ya sayansi ni wajibu wa mlezi pamoja na jamii kuwaahamasisha na kuwatia moyo wanafunzi kusoma masomo hayo kuanzia ngazi za chini kabisa.

Alisema kuwa kila mwanafunzi anahitaji kusoma masomo ya sayansi kwa kupata vitendo kwa nadharia zaidi ili aweze kufahamu anachokisoma, hivyo serikali kupitia masihirika na Taasisi mbalimbali zinajitahidi kumfikishia mwanafunzi vifaa vya majaribio kwa lengo la kutochukia masomo ya sayansi yanayohitaji vitendo .

Pia, alisema Wizara ya elimu pamoja na Taasisi zinazoshughulika na masomo ya sayansi zinaanzisha mashindano ya masomo ya sayansi kila mwisho wa mwaka ili kuhamasisha vijana kupenda masomo hayo na Taifa kuzidi kupata wataalamu wa mambo ya sayansi.

“Tutaanzisha mashindano maalum ya masomo ya sayansi kwani bila ya mashindano hakutakuwa na mafanikio ya masomo haya hivyo vijana wetu lazima wasome kemia, biology, physics pamoja na somo la hesabu” alisisitiza Mbarawa