Na Thomas Dominick wa Binda News-Musoma
HALI bado ni tete katika Hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya Wauguzi wa Hospitali hiyo kugoma tena kushinikiza kulipwa fedha zao za kuitwa kufanya kazi baada ya kazi. Mgomo huo ulianza Mei 25 mwaka huu ambapo baada ya vuta ya huku na kule wauguzi hao waliamua kurudi kazini kwa makubaliano kuwa siku ya Jumanne Mei 29 watapata suluhu ya madai yao baada ya kuunda tume ambayo itayapitia madai yao.
Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali Watu, Buhacha Baltazary aliwaombqa wauguzi hao warudi kazini huku ofisi yake ikishughulikia tatizo lao hilo na baada ya muda watapewa majibu.
“Turudi kazini kwanza hapa tumekuja ili tutatue tatizo lenu hili mapema lakini tanataka muende mukawaudumie wagonjwa ambao wamekuja kupata matibabu baada ya kukamilisha tutawaita na kuongea nanyi,” alisema Baltazary.
Lakini hali haikuwa kama walivyotarajia baada ya tume hiyo iliyokuwa china ya Katibu wa TUGHE Mkoa wa huo ambaye ni Mwenyekiti wa Tume Watson Rushakuzi baada ya kukutana na wauguzi hao kuwaomba waingie kazini hadi watakapo kamilisha kazi yao ambao walikataa kabisa kuingia kazini hadi madai yao yaishe.
“Ndugu zangu tume ambayo mliichagua tangu Ijumaa bado haijakamilisha kazi yake huvyo ingieni kazini kwanza na baada ya masaa mawili tutawaita kuwapa suluhu iliyofikia sambamba na kuwaambieni juu ya malipo yenu,” alisema Rushakuzi.
Kutokana na kauli hiyo wauguzi hao walikuja juu na kudai kuwa katika masaa hayo mawili ya kukamilishwa kwa kazi hiyo watasubiria nje na kamwe hawataingia wodini kufanya kazi hadi kieleweke.
“Hatutaingia kazini kama mumeamua kuja kutudanganya kama watoto sisi ni watu wazima tutawasubirieni hapa hapa kwani masaa mawili sio mengi naomba mtuelewe hatuingii kazini hadi kieleweke leo hii,” alisema Neema Chacha ambaye ni Muuguzi.
Baada ya maneno hayo ya muuguzi huyo wauguzi wote walilipuka na kuanza kuimba, “tumechoka kuonewa kunyanyaswa na mafisadi, Tumechoka na Ufisadi, nyimbo ambazo zilimfanya Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali watu Buhacha Baltazary kuondoka.
Inadaiwa kuwa kuna fedha iliyoletwa kwa ajili ya malipo ambayo ni sh. Milioni 48 kwa ajili ya malipo ya watumishi hao ambapo zilizolipwa ni milioni 14 ambazo waliolipwa ni pamoja na wataalamu bigwa, madaktari, wataalamu wa afya na baadhi ya wauguzi.
Historia ya hospitali hiyo hii ni mara ya kwanza kwa watumishi wa Hospitali hiyo kuingia kwenye mgomo tangu ilipoanzishwa miaka ya 1939 hawajawahi kuingia kwenye mgomo wowote ambapo baadhi ya Hospitali nchini ikiongozwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuingia kwenye migomo kila mara kwa ajili ya kudai haki zao.