CCM Kibaha yawacharukia watendaji

 

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Bw. Wilson Mukama

Na Mwandishi Wetu
Kibaha

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini kimewacharukia watendaji wa ngazi mbalimbali katika halmashauri ya mji huo kutokana na baadhi yao kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Maulid Bundala kwenye kikao cha madiwani kilichofanyika juzi mjini hapa, ambapo alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakiwashutumu watendaji hao.

Alisema kutokana na ukweli huo yamekuwa yakiibuka malalamiko mengi jambo ambalo uongozi huo hauwezi kulifumbia macho na kuwaomba wasioweza kutekeleza majukumu yao wakae kando.

“Watendaji wote katika idara mbalimbali ndani ya halmashauri wengi wenu mmekaa kwenye nafasi hizo kupitia CCM, hivyo kutotekeleza ipasavyo majukumu yenu mnakisababishia lawama chama hiki,” alisema Bundalla.

Kauli hiyo iliungwa mkono pia na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba ambaye alieleza kuwa amekuwa akipokea malaamiko mengi kutoka kwa wananchi wakiwalalamikia watendaji wa ngazi mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo.

“Umefika wakati sasa kwa kila mmoja wetu kutekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa, kwani kinyume chake inawakatisha tamaa wananchi wetu,” alisema Kihemba.

Hata hivyo, kwa upande mwingine Kihemba aliwataka watendaji hao kutekeleza majukumu ya kuwatumikia wananchi kwani kinyume chake inawakatisha tamaa wanachi na kupoteza imani na serikali na chama chao cha Mapinduzi.