Kiongozi wa Uamsho aachiwa kwa dhamana Zanzibar

Hata hivyo, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, imekana kuhusika na machafuko yote yaliyotokea

HALI sasa ni shwari na kwamba shughuli za maisha zimearudi kama kawaida. Viongozi wa jeshi la polisi, wanasiasa, na wa jumuiya za kidini wamo kwenye mikutano ya kutuliza hali na kujenga tena mazingira ya kuaminiana na kufanya kazi pamoja.
Akizungumza na Deutsche Welle kwa njia ya simu kutokea Zanzibar hapo jana, Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali, alisema hali sasa imedhibitiwa.
“Mji wa Zanzibar sasa uko kwenye utulivu na polisi inahakikisha kuwa hakuna matatizo yoyote yanayoweza kuwavunjia watu shughuli zao.” Amesema Kamishna Mussa.
Kamishna huyo alikanusha taarifa zilizokuwa zimezagaa kwamba helikopta za jeshi lake zimekuwa zikifyatua mabomu ya machozi kwa vikundi vya waandamanaji, akisema kwamba helikopta hizo zimekwenda tu na maafisa wa polisi kutoka Tanzania Bara kwa mashauriano ya kiusalama.
Kuzorota kwa hali ya usalama kulianza jioni ya jana, baada ya polisi kumkamata mmoja wa wahadhiri wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, Maalim Mussa, wakimhusisha na maandamano yaliyofanywa mchana wa jana kuzunguka mji huo, na wafuasi wa jumuiya ya uamsho.
Viongozi wa maandamano hayo, walisema baadaye kwamba walikusudia kupeleka ujumbe kwa serikali za Zanzibar na Tanzania, kutaka iitishwe kura ya maoni kuamua hatima ya Muungano wa Tanzania.
Machafuko ya hapo usiku yalipelekea kuchomwa moto kwa mali, magari na kanisa moja, lililoko kando kidogo ya kitovu cha mji wa Zanzibar. Akizungumzia mkasa huo, mchungaji Dickson Kaganga wa kanisa hilo amesema kwamba watu wasiojuilikana walilivamia kanisa lake usiku wa saa 4:00 kwa majira ya Afrika Mashariki na kulitia moto. Gari ya mchungaji huyo ni miongoni mwa mali kadhaa zilizoharibiwa mjini Zanzibar.
Hata hivyo, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, imekana kuhusika na machafuko yote yaliyotokea kuanzia hapo jana. Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Abdallah Said, ameiambia Deutsche Welle kwamba Uislamu ni dini ya amani na unaamrisha kulindwa kwa nyumba za ibada, na hivyo haielekei kwa jumuiya yake kwenda kinyume na dini wanayoiamini na kuihubiri.
Hadi mchana bado polisi walionekana wakitembea katika magari ya deraya na mabomu yalisikikana katika maeneo kadhaa mjini Zanzibar. Shahidi mmoja aliye mjini Zanzibar ameiambia Deutsche Welle kwa njia ya simu kwamba polisi walipiga mabomu ya machozi kwenye eneo la soko kuu la vyakula, Mwanakwerekwe, kando kidogo ya mjini Zanzibar.
Sekta ya utalii inayotegemewa kwa kiasi kikubwa na uchumi wa Zanzibar inahofiwa kuathrika ikiwa machafuko yataendelea. Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2010, Zanzibar imekuwa kwenye shuwari isiyo ya kawaida, baada ya Maridhiano kati ya waliokuwa mahasimu wakubwa wa kisiasa, vyama vya CCM na CUF, na kura ya maoni iliyobariki kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi huo. Huu ni mtihani wa kwanza wa kisiasa kwa serikali hiyo iliyodumu sasa miaka miwili.

-DW