Arusha mwenyeji Mkutano wa Utawala Bora Afrika

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini

Na Mwandishi wetu-Arusha
ZAIDI ya wajumbe 80 kutoka kanda tano za Afrika watakusanyika mjini Arusha, Jumatano ijayo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Nane wa Afrika wa Utawala Bora.
Kwa mujibu taarifa kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mkutano huo wa siku mbili utafunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Dk. Richard Sezibera. Kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘’Demokrasia, Uchaguzi na Utawala Bora Afrika.’’
Lengo la msingi la mkutano huo ni pamoja na kuchambua na kujadili hali ya demokrasia, uchaguzi na utawala bora katika kila kanda ya Afrika ikiwa ni pamoja na kanda za Kati, Mashariki,Kaskazini,Kusini na Magharibi.
Majadiliono yatazingatia maendeleo yaliyofikiwa juu ya mchakato mzima wa mwelekeo wa demokrasia barani Afrika, kutambua changamoto zilizobaki, kuchukua uzoefu bora ulipopatikana na kupendekeza sera madhubuti ya kufikia malengo.
Mgeni rasmi katika mkutano huo ni Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi wa Nchi za Ushirikiano wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Wakili Pansy Tlakula.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya EAC, Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (ECA).
Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Jukwaa la Nane la Afrika la Utawala Bora ambao umepangwa kutanyika Novemba 2012.