Wabunge wawaadhibu wakuu wa idara Kisarawe

Mbunge wa CCM, Idd Azan

Na Mwandishi Wetu
Kisarawe

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LACC), juzi imewapa wakuu wa idara anuai za Kisarawe adhabu ya kukatwa mishahara yao ya mwezi ujao kutokana na kile kutoa taarifa za uongo katika miradi ya maendeleo za mwaka 2008/09.

Hayo yalisemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Idd Azan, alipokuwa akitoa taarifa za ukaguzi za miaradi hiyo juzi mjini hapo.

“Mmetoa vitabu vyenye kumbukumbu za uongo juu ya miradi hiyo, na tumepitia miradi ya aina mbalimbali na kugundua kuwa taarifa zilizopo katika vitabu hivyo si sahihi…taarifa zenu ni za uwongo. Kamati inawapa adhabu ya kukatwa tuzo ya mshahara wa wezi ujao kwa wafanyakazi wa halmashauri ili iwe fundisho dhidi ya tabia ya kusema uwongo,” alisema.

Aidha alifafanua kuwa licha ya kukatwa kwa wafanyakazi hao, wafanyakazi Juliet Kalengi na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), Msangi Mwendo hawatahusika na adhabu hiyo kwani wao ni wageni eneo hilo la kazi.

Azan alimtaka DMO, Mwendo kuwa makini na suala zima la utoaji taarifa na anatakiwa kuwa na hakika kwa kila taarifa anazo toa. Akielezea Mbunge Azan alisema kuwa miradi mingi ya Kisarawe inamatatizo na hali ya ukaguzi haikuwa ya kuridhisha kutokana na tofauti kuwa kwenye vitabu.

Alibainisha kuwa miradi imeonekana kutolewa taarifa za mkanganyiko kiasi cha kuonekana wazi kuna udanganyifu umefanywa. Amesema baadhi ya miradi katika vitabu imeonesha kufanyika mwaka 2008 hadi 2009, lakini miradi hiyo ilitakiwa tangu mwaka 2006.

Pia amewataka madiwani kutumia nafasi zao kuwahamasisha wananchi ili wajue jinsi ya kuchangia katika miradi ya maendeleo.
Akizungumzia mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wa 2008 hadi 2009, alisema mradi huo ulikuwa wa 2007, hivyo kumtaka mkaguzi afanye hesabu kujua fedha za mradi huo zilikwenda wapi.

Pamoja na hayo alimtaka mkaguzi kupitia vizuri taarifa zote ili kupata uhalari wa fedha zilizotumika na kama si sahihi wahusika wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.

Katika ziara hiyo ya Kamati ya LACC, wajumbe walifanikiwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kubaini upungufu mkubwa, hivyo kufikia uamuzi wa kutaka wafanyakazi wa halmashauri kukatwa mishahara.