Na mwandishi wetu,Kilimanjaro
WATU wanoishi na Virus vya ukimwi (VVU) hapa nchini wametakiwa kuwa
wazi na kuepuka kuwaambukiza wengine virusi hivyo, hatua ambayo
itafanikisha jitihada za serikali za kupunguza maambukizi mapya ya
ugonjwa huo hatari.
Mbali na watu hao kuwa wazi pia viongozi wa dini hapa nchini,
wametakiwa kujitokeza kupima afya zao ili kuweza kujitambua na kuwa
mfano kwa waumini wao na kutoa elimu hali ambayo itasaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza kasi ya maambukizi ya ukimwi.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mratibu wa shirika lamtandao
wa viongozi wa dini wanaoishi na virusi vya ukimwi Tanzania
(TANERELA),Mchungaji Amini Sandewa, wakati akizungumza kwenye
mkutano wa kuadhimisha miaka mitatu kwa benki ya Kijamii VIKOBA
wilayani Rombo iliyoko chini ya shirika hilo.
Mch. Sandewa alisema njia sahihi ya kutokomeza maambukizi mapya ya
virusi vya ukimwi ni wale waliokwisha pata maambukizi kuwa wazi na
kuhakikisha hawawaambukizi watu wengine virusi hivyo.
“Njia sahihi ya kutokomeza maambukizi ya ukimwi hapa nchini ni wote
ambao wameshapata ugonjwa huu kuwa wazi na kuweka dhamira ya
kutowaambukiza watu ambao hawajaupata lakini pia wale ambao hawajapata
maambukizi wajilinde na kuhakikisha hawapati maambukizi”alisema Mch.
Sandewa.
Aidha alisema ni jukumu la viongozi wa dini kutoa elimu katika jamii
kuhusiana na maambukizi ya VVU na kwamba hilo litawezekana endapo nao
viongozi watapima afya zao na kujitambua ili kuwa mfano kwa waumini
wao.
“Ninyi viongozi wa dini mnanafasi kubwa sana ya kuwaelimisha wananchi
juu ya gonjwa hili hatari wakiwemo wanandoa vijana na jamii kwa ujumla
na ili kuweza kuyafikia malengo ya kupunguza kasi ya maambukjizi ya
ukimwi nanyi pia hamna budi kupima na kuwa wazi juu ya afya
zenu”alisema Sandewa.
Awali akizungumza Mratibu wa Vicoba Wilayani Rombo Mch. Nicolaus
Kimario,aliwataka viongozi wa kata na vijiji katika wilaya hiyo
kuwahamasisha wananchi wilayani humo kujiunga kwenye Benki ya vikundi
vya Kijamii (VICOBA) hatua ambayo itawawezesha kupata mikopo na
kuanzisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo itawakwamua kiuchumi
na kuwaondoa katika lindi la umaskini.
Naye Afisa Tarafa ya Mkuu wilayani Rombo Bi. Sarah Masaoe ambaye
alimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo aliitaka benki hiyo kuongeza juhudi
katika uhamasishaji wananchi kujiunga na Vicoba hatua ambayo
itawezesha wananchi wengi zaidi kuhamasika na kujikwamua kiuchumi.