SERIKALI imejipanga kupunguza kwa zaidi ya asilimia 90 tatizo la ukosefu wa walimu linalozikabili shule za sekondari za kata nchini ifikapo mwaka 2014.
Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya elimu Kassim Majaliwa amesema tatizo la upungufu wa walimu wapatao 37,784 limeanza kushughulikiwa ambapo walimu 13,000 wamepelekwa kwenye shule hizo mwanzoni mwa mwaka huu.
“Hapa nchini kuna jumla ya shule za sekondari za umma zipatazo 3,340 kati ya hizo zaidi ya 2,850 ni zile zilizojengwa na jamii kwenye kata”.
Amesema walimu wengine zaidi ya elfu kumi watakaohitimu na kufaulu kutoka katika vyuo vikuu nchini mwaka huu pia wanatarajiwa kupelekwa kwenye shule hizo kabla ya mwisho wa mwaka.
Kiongozi huyo amesema katika kutimiza azma yake hiyo ya kumaliza tatizo la walimu katika shule za sekondari za umma nchini serikali iliviomba vyuo vikuu vya binafsi nchini kutoa kipaumbele kufundisha kozi ya ualimu.
Katika mahojiano kwa simu na TAMWA mwishoni mwa wiki Majaliwa alisema serikali imejipanga kuhakikisha kwamba kila mwalimu anapata mshahara wake kwa wakati.
Amesema maafisa utumishi katika halmashauri za wilaya zote 133 nchini zimeshaagizwa kuhakikisha kuwa taarifa za walimu wote zinaingizwa kwenye mtandao wa malipo hazina ili kila mwalimu aweze kupokea mshahara wake kwa wakati kupitia akaunti yake ya benki.
Amewahimiza walimu wapya wote wanaoajiriwa kuhakikisha wanapokwenda kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi wanakwenda wakiwa na taarifa zao zote muhimu hasa vyeti na namba za akaunti zao ili kuhakikisha zoezi la kuwaingiza kwenye malipo hazina linafanyika kwa wakati.
Majaliwa ameonya kwamba halmashauri itakayozembea jambo hilo kwa kisingizio chochote itakuwa imetangaza mgogoro na serikali na kwamba kama kuna halmashauri ina tatizo la kuingiza majina ya walimu katika mtandao wa malipo hazina iombe kutumia mtandao katika wilaya nyingine au mkoani.
Kuhusu nyumba za walimu Majaliwa amezihimiza halmashauri zote nchini kujiwekea mipango maalum itakayowezesha kila shule ya sekondari ya kata kuwa na nyumba za kutosha walimu wake ifikapo mwaka 2014.
Amesema mwaka huu wa fedha serikali ilitenga shilingi bilioni 4.4 ambazo zilisambazwa kwenye halmashauri zote kwa makisio kwamba nyumba moja ya mwalimu ingegharimu shilingi milioni 15.
Kadhalika Majaliwa amesema wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) mwaka huu imepeleka jumla ya shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya kujenga maabara ya masomo ya Biolojia, Fizikia na Kemia.
Amewataka madiwani kuwa makini kufuatilia fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri kwa ajili ya kuimarisha shule ili kuhakikisha zinatumika zote kwa shughuli zilizokusudiwa.
Kuhusu tatizo la chakula mashuleni ambalo ni chanzo kikubwa cha ongezeko la mimba na wanafunzi kufeli amesema atalitolea tamko baada ya kukusanya takwimu.
Utafiti uliofanywa na TAMWA katika wilaya 20 nchini mwanzoni mwa mwaka huu ulibaini kuwa wanafunzi wengi za shule za sekondari za kata wanakatiza masomo na kufeli kutokana na ukosefu wa walimu.
Utafiti huo ulibaini kuwa walimu wanaopelekwa katika shule hizo hawakai kutokana na mishahara yao kucheleweshwa, ukosefu wa nyumba za kuishi, maji, umeme na barabara za kufika kwenye shule zao.