Maadhimisho ya siku ya Afrika yafana, London

Ngoma kutoka Ghana ilitumbuiza nakuwafanya watu wote kujisikia nyumbani

Na mwandishi wetu London Uingereza
Siku ya Afrika iliadhimisha rasmi jana hapa nchini Uingereza kwa kujumisha nchi zote za Afrika zenye Balozi au Wawakilishi wao hapa nchini Uingereza. Katika sherehe hiyo rasmi ya kuadhimishwa kwa Siku ya Afrika, kulitolewa hotuba na Balozi wa Botswana na mbaye ni Mkuu wa Mabalozi wa nchi za Afrika hapa Uingereza, Mheshimiwa Roy Warren Blackbeard.

Aidha Balozi Roy Blackbeard, alitoa salamu maalum kutoka kwa mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa nchi za Afrika, Mheshimiwa Yayi Boni, ambaye pia ni Rais wa Benin.

Balozi Roy, alielezea changamoto nyingi zinazo tokea Barani Afrika na kwingineko na juhudi maalum zinazofanywa na Jumuiya ya Umoja wa nchi za Afrika kutatua migogoro na matatizo ya mara kwa mara yanayolikumba Bara letu la Afrika.

kabla ya kutolewa hotuba hiyo, Balozi wa Uganda Mheshimiwa Mama Joan Rwabyomere, alifungua kwa kuwakaribisha Mabalozi, Wawakilishi, Marafiki wa Afrika na Wageni mbalimbali waalikwa na kuwashukuru kwa kufika kwao na kujumuika pamoja na waafrika wote duniani kuadhimisha siku hiyo hapa nchini Uingereza. Amani, Upendo, Ushirikiano na Mshikamano miongoni mwa nchi za Afrika vilihimizwa katika maadhimisho hayo.