Na mwandishi wetu Kilimanjaro
HIFADHI ya taifa ya mlima Kilimanjaro (KINAPA) imewakamata watu 12 kwa tuhuma za kuhusika na uvunaji haramu wa miti katika hifadhi hiyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria
Mbali na watu hao pia hifadhi hiyo imekamata Mbao 2,889 na Nguzo Nne ambazo zimevunwa katika hifadhi hiyo kinyume cha sheria pamoja na Chainsaw Nne na misumeno Mitatu ambazo zilikuwa zikitumiwa katika uvunaji wa miti hiyo.
Hayo yalibainishwa na mhifadhi mkuu wa Kinapa Bw.Erastus Lufungulo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi katika mlima Kilimanjaro ambayo inaendeshwa na Kinapa kwa kuwashirikisha wananchi kutoka vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Bw. Lufungulo alisema watu hao walikamatwa kufuatia Doria maalumu iliyofanyika maeneo mbalimbali ya Marangu kati ya April 24 na Mai 25 mwaka huu.
“Tulifanya doria maalumu ya upekuaji na katika doria hii tulikamata mbao nyingi sana pamoja na majangili wanaohusika na uharibifu katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro”alisema Bw. Lufungulo.
Alisema Mbao 2,889 zilizokamatwa ni pamoja na Gevelia 1005,Mfuruanje 1002,Cypres 16,Eucalyptus 398, Parachichi 170, Podo 219,Zyzygium 79 pamoja na Nguzo nne za Mndiri.
Akizungumzia kampeni ya usafi Bw. Lufungulo alisema suaa la usafi katika mlima Kilimanjaro ni la muhimu sana kutokana na umuhimu wa mlima huo katika nchi na hata nje ya nchi.
“Kuzindua kampeni hii Leo hakuna maana kwamba mlima huu ulikuwa haufanyiwi usafi,ni kwamba mazingira ya mlima huu yanafanyiwa usafi kila wakati lakini leo tumeamua kuzindua kampeni hii ili kushirikiana na wananchi wanaozunguka hifadhi hii, na hatua hii itasaidia kuweka mazingira ya mlima kuwa safi wakati wote na kujenga uelewa zaidi kwa wananchi”alisema Bw.Lufungulo.
Akizindua kampeni hiyo ya usafi katika mlima Kilimanjaro kaimu katibu tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Gadson Lengwana alisema suala la usafi katika hifadhi ya Kinapa ni la muhimu sana kutokana na kwamba hifadhi hiyo imekuwa ikikabiliwa na tatizo kubwa la uchafu kwa kipindi kirefu hali ambayo imekuwa ikisababishwa na wapagazi wanaopanda mlima huo kutupa taka ngumu zisizo oza kama vile mifuko ya plastiki.
Alisema suala la uchafu katika mlima Kilimanjaro linapaswa kuangaliwa na kukomeshwa kutokana na kwamba hali hiyo inaweza ikaleta madhara makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Hifadhi ya taifa imeonelea umuhimu wa kufanya kampeni ya usafi wakati wageni ni wachache na hali hii itasaidia kuweka mazingira ya mlima huu kuwa safi kwani endapo uchafu utazagaa katika mlima huu utaleta madhara makubwa na utasababisha watalii wasije kwa wingi jambo ambalo ni hatari sana”alisema Bw. Lengwana.
Jumla ya watu 96 walipanda mlima huo kwa ajili ya kufanya usafi ambapo 90 wanatoka katika vijiji vya Machame,Umbwe,Mweka,Marangu,Rongai na Londros huku wengine Sita wakiwa ni viongozi.