KUHUTUBIA JANGWANI, POLISI YAKATAA OMBI LA CHADEMA KUANDAMANA
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa leo wanatarajiwa kuhutubia wanachama na mashabiki wa chama hicho katika mkutano mkubwa uliopangwa kufanyika katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Mbowe alisema jana kwamba mkutano huo unalenga pamoja na mambo mengine, kuwaandaa kisaikolojia wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kukipokea chama chake kuingia Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alijigamba kwamba Chadema hakina shaka kwamba kitashinda Uchaguzi Mkuu ujao na kuunda Serikali, hivyo kinapaswa kuwaandaa watu kisaikolojia. Huu ni mkutano mkubwa wa kwanza wa Chadema kufanyika Dar es Salaam baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010. Unafanyika kipindi ambacho wapenzi na wanachama wake wakiwa bado wanasherehekea ushindi wa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika katika hukumu ya kupinga matokeo yake ya ubunge iliyotolewa juzi na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa wameruhusu kufanyika kwa mkutano huo, lakini wakazuia maandamano kutokana na kile alichodai kuwa ni kutokuwa na askari wa kutosha.
Vuguvugu la Mabadiliko Mbowe alisema katika mkutano huo, viongozi wa chama hicho watawaeleza wananchi namna Programu ya ‘Movement for Change’ (Vuguvugu la Mabadiliko) inavyofanya kazi.
Alisema Chadema kimeanzisha Programu ya Movement for Change ili kuwahamasisha wananchi kujiunga na chama hicho na kuendeleza maono ya kuusaka uongozi wa nchi mwaka 2015. Pia alisema kwamba mkutano huo utatumika kuzindua rasmi mpango wa kitaifa wa kukichangia chama hicho, ili kujenga uwezo wa kujiendesha sasa na siku zijazo. “Tutawaeleza wananchi wawe tayari kwani chama chao kina kila sababu ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015. Pia wafahamu nini wanachotakiwa kufanya kwa sasa katika maandalizi hayo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunataka wananchi, Watanzania wawe sehemu ya mabadiliko tunayoyakusudia kuyafanya katika nchi yetu, wawe wamiliki wa mabadiliko hayo. Sasa watashiriki vipi? Ndiyo jambo tunalokwenda kuwaambia kesho.” Katika hatua nyingine, Mbowe alisema viongozi wa Chadema watatumia fursa hiyo kuwaeleza wanachama na wafuasi wao msimamo wa uongozi katika upatikanaji wa Katiba Mpya.
CHANZO: Mwananchi, kusoma zaidi habari hii bofya http://www.mwananchi.co.tz/