Njaa bado tatizo nchi za Afrika-Janet Mbene

Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene (MB) akisoma hotuba wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2012. Kushoto ni Mkurugenzi wa UNDP Tanzania, Phillipe Poinsot.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa UNDP nchini Tanzania Dk. Alberic Kacou akizungumza kwa niaba ya UNDP kuhusiana na kuzinduliwa kwa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2012 ambapo amesema huu sasa ni wakati kwa nchi za Afrika haswa zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara kujenga mazingira ya kuelekea mustakabali wenye uhakika wa chakula. Picha zote na MO BLOG

Njaa bado tatizo nchi za Afrika-Janet Mbene

Na Mwandishi Wetu

BARA la Afrika ikiwemo Tanzania limeshakumbwa na matukio ya uhaba wa chakula, uliosababisha watu wengi kupoteza maisha hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara na Ukanda wa Sahel eneo la Afrika Magharibi.

Hali hiyo imekuwa moja ya changamoto kubwa inazozikabili Serikali za mataifa hayo ambapo yanapambana kuitatua ili kila mwananchi barani Afrika aweze kufurahia kukua kwa uchumi katika taifa lake.

Akitoa hotuba wakati akizindua rasmi Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2012 jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene (MB) amesema kwa muda mrefu sura ya eneo la nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara imekuwa ni ya njaa ya kukithiri, ambapo zaidi ya mtu mmoja katika kila waafrika wane wana tatizo la upungufu wa lishe.

Pichani Juu na Chini ni Baadhi ya Maofisa wa Umoja wa Mataifa na Wadau wa Serikali wakichangia maoni yao kuhusiana na Ripoti hiyo.


Amesema ripoti hiyo inaonesha kuwa pamoja na ukweli kwamba baadhi ya nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi katika kipindi cha miaka kumi ziko Afrika, lakini bado hali ya maisha ya waafrika ni duni.

Awali Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa UNDP nchini Tanzania Dk. Alberic Kacou alisema bara la Afrika limejaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba, maji ya kutosha na hali nzuri ya hewa kwa kukuzia mazao, lakini swali la kujiuliza ni kwanini bado kuna uhaba wa chakula.

Hata hivyo Dk. Kacou ametoa matumaini kuwa bara la Afrika bado lina uwezo wa kujijengea mazingira ya kuwa na akiba ya kutosha ya chakula kwa kipindi kijacho. Ripoti hii ya Kwanza ya Maendeleo ya Afrika inasema kwamba ongezeko endelevu katika uzalishaji kwenye kilimo kunalinda haki ya chakula na uwezo wa watu kupata chakula.