Waliokufa ajali ya mbunge Moshi waongezeka

Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasin aliepata ajali mjini Moshi

Mwandishi Wetu, Thehabari-Moshi

IDADI ya watu waliofariki dunia katika ajali ya gari la Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasin kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imeongezeka na kufikia watu wanne baada ya majeruhi mmoja kufariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Ajali hiyo ambayo iliyotokea Mai 24 majira ya Saa moja usiku eneo la Bomang’ombe Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ilisababisha watu watatu kufa papo hapo na mmoja alifariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya KCMC hivyo kusababisha idadi ya waliokufa kufikia wane na majeruhi Wawili ambao ni Mbunge na mke wake.

Gari hilo lenye namba za usajili T.441BRT aina ya Toyota Land Cruiser VXR S/Wagon likiendeshwa na Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasin (50) mkazi wa Rombo lilikuwa likitokea mkoani Arusha kuelekea wilayani Rombo ambapo lilikuwa limebeba abiria Sita ambao ni wanafamilia.

Akizungumzia ajali hiyo Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea Mei 24 majira ya saa moja usiku wakati mbunge huyo akitokea mkoani Arusha awalikokuwa wamekwenda kwenye msiba kuelekea nyumbani kwake wilayani Rombo.

Kamanda Mwakyoma alisema gari hilo lilipofika eneo la Chuo cha ufundi Bomang’ombe barabara kuu ya Mosh/Arusha liliacha barabara na kuhamia upande wa kulia na kupinduka baada ya kugonga kalvati na kusababisha vifo vya watu wanne ambapo kati yao watatu walifariki papo hapo.

Kamanda Mwakyoma aliwataja waliofariki kuwa ni Katherini Roman Selasin(80)ambaye ni mama mzazi wa Mbunge huyo, Mariana Kisela mwenye umri kati ya miaka (70-75), Angelindis Masawe mwenye miaka kati ya (35-40) pamoja na Agatha Jerome (85) ambaye alifariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa KCKC.

Amewataja majeruhi kuwa ni Digna Kavishe (43) ambaye ni mke wa Mbunge, Joseph Selasin, ambapo ameumia kichwa na hali yake ni mbaya pamoja na mbunge huyo ambaye ameteguka Bega la mkono wa Kulia na hali yake sio mbaya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamanda Mwakyoma Chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na kwamba uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo bado unafanyika. Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC kwa ajili ya matibabu na maiti pia zimehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Akizungumza katika hospitali ya Rufaa ya KCMC anakopata matibabu mbunge Selasini alisema anaendelea vizuri licha ya kuwa bado anasikia maumivu katika kifuua, mgongo na kiuno.