Bin Hammam, Warner wachunguzwa kwa rushwa

SHIRIKISHO la Soka Ulimwenguni (FIFA) imeanza uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazozingira maafisa wake, akiwemo makamu wa rais Jack Warner na mgombea wa kiti cha urais wa Fifa Mohamed bin Hammam.

Tuhuma hizo zilitolewa na mjumbe wa kamati kuu Chuck Blazer. Blazer amedai taratibu za maadili ya Fifa zilikiukwa katika mkutano unaoonekana uliandaliwa na Bin Hammam na Warner.

Maafisa wengine wawili ni Debbie Minguell na Jason Sylvester kutoka Muungano wa Soka wa nchi za Caribbean.

Mkutano uliofanyika tarehe 10 na 11 mwezi wa Mei, ulihusiana na uchaguzi wa rais wa Fifa utakaofanyika tarehe 1 mwezi wa Juni.

Bin Hammam, rais wa Shirikisho la Soka la Asia, anawania nafasi ya urais wa Fifa dhidi ya rais wa sasa Sepp Blatter, akitafuta nafasi ya kuwa kiongozi mpya wa shirikisho hilo la soka duniani.

Maafisa hao wanne wameitwa kufika mbele ya kamati ya maadili ya Fifa mjini Zurich tarehe 29 mwezi wa Mei.

Fifa imetangaza Claudio Sulser, mkuu wa kaamti ya maadili, hataongoza kikao hicho kwa vile ni raia wa Switzerland sawa na Blatter ambaye ni mpinzani wa Bin Hammam.

Badala yake kikao hicho kitakuwa chini ya naibu mwenyekiti Petrus Damaseb wa Namibia.