Marais wastaafu nchi nne Afrika wakutana Afrika Kusini

Marais wa nchi nne Afrika katika picha ya pamoja

Na Michuzijr Blog-Johannesburg

MARAIS wastaafu nane wa nchi za Afrika wamekutana jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kufanya mkutano wa siku tatu ndani ya Chuo Kikuu cha Witwatersrand. Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kujadili maendeleo ya matumizi ya nishati karne ya 21 kwa nchi za Afrika.

Marais wastaafu hao waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria, Rais Ali Hassan Mwinyi wa Tanzania, Rais Nicéphore Dieudonné Soglo wa Benin, Rais Pedro Pires wa Cape Verde, Rais Benjamin Mkapa wa Tanzania, Rais Joaquim Chissano wa Msumbiji, Rais Amani Abeid Karume wa Zanzibar na Rais Rupiah Banda wa Zambia.

Aidha – mbali ya Marais hao waliohudhuria mkutano huo, pia ulihudhuriwa na Wataalam mbalimbali wa nishati, viongozi wa umma na sekta binafsi na wanafunzi na kitivo kutoka vyuo vikuu 9 vya kimataifa kikiwemo chuo kikuuu mwenyeji cha Witwatersrand a.k.a Wits. Tanzania iliwakilishwa na wanafunzi watano na walimu wawili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mratibu mkuu wa mkutano huo – Balozi Charles Stith ambaye aliwahi kuwa balozi wa Marekani nchini Tanzania alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadiliana juu ya ufumbuzi wa mageuzi ya nishati katika nchi za Kiafrika, na kuhakikisha nchi za Afrika zinajiwakilisha vyema katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika suala zima la Nishati.

Balozi Stith alisema kuwa mkutano huo utaleta mshikamano wa pamoja kwa viongozi wa sekta ya nishati na wafadhili mbalimbali wa miradi mbalimbali, ili kuhakikisha nishati hiyo inatosheleza mahitaji ya Afrika kwa ujumla.Mkutano huo wa siku 3 utafikia tamati Mei 25.