Na Magreth Kinabo wa MAELEZO DSM
TANZANIA imefanikiwa kupunguza idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa Malale kutoka wagonjwa 380 mwaka 1996 hadi kufikia wagonjwa wawili katika kipindi cha mwaka jana.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Dk. Geoffrey Kiangi kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali katika semina ya siku moja ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari juu ya ugonjwa wa Malale iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Utafiti wa Kinga na Tiba wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) jijiini Dar es Salaam.
“Haya ni mafanikio makubwa katika jitihada hizi kutokomeza mbung’o na Malale na kuufanya kuwa ni historia katika nchi yetu,” alisema Dk. Kiangi.
Aliongeza kuwa anapenda kuwapongeza wadau wote kwa mafanikio yaliyoptaikana na Serikali kwa kuwapatia wafugaji dawa za ruzuku za uogeshaji wa mifugo mabazo zimechangia kuua mbung’o katika maeneo mengi ya wafugaji.
Dk. Kiangi aliwataja wadau hao kuwa ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Wizaraya Maliasili na Utalii(TANAPA), Shirikala Afya la Dunia(WHO) na Umoja wa Afrika katika mpango wake wa Kutokomeza Mbung’o na Ndorobo uitwao “Pan African TseTse and Trypanosomias Eradication Campaign (PATTEC).”
Aliyataja maeneo yanayoathiriwa na ugonjwa huo kuwa ni Tabora, Rukwa, Kigoma, Mara, Arusha, Mbeya na Manyara, kwa upande wa wanyama huitwa Nagana na umesambaa katika mikoa yote husababisha hasara kubwa katika ukuaji wa uchumi na kipato cha familia na umekuwa ukiathiri watu wa kipato cha chini na wanaoishi katika maeneo ya vijijini karibu na misitu.
Dk. Kiangi alisema Tanzania imeathirika na wadudu aina ya mbung’o kwa asilimia 65 na kufanya watu milioni nne na mifugo milioni saba kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa Malale (binadamu) na Nagana (wanyama). Alisema mfano wafugaji nchini hupoteza takribani sh. bilioni 12.7 kwa mwaka kutokana na mifugo yao kufa na kupunguza uzalishaji wa maziwa na bidhaa zinazotokana na mifugo.
Naye Mtaalamu mwingine kutoka wizara hiyo, Charles Mwalimu alitoa wito kwa wataalamu wa afya kufanya uchunguzi wa damu kwa ajili kutambua vimelea vya ugonjwa wa malale wakati wanapopiima wa kutambua ugonjwa wa ugonjwa wa malaria ili kuiwezesha Tanzania kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa huo na kupunguza athari zake.
Alizitaja baadhi ya athari hizo kuwa ni kifo, kupungua kwa nguvu kazi, kiuchumi, kupungua kwa watalii, kuathirika kwa mfumo wa fahamu, kuvunjika kwa ndoa na unyanyapaa. Aliwataka wananchi kufika katika vituo vya afya ili kuweza kupata tiba mapema ili kupunguza athari zake.