RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Massawe kuomboleza kifo cha Mzee Dk. Vedastus Nshunju Kyaruzi ambaye aliaga dunia mwishoni mwa wiki kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba baada ya ugonjwa wa muda mfupi.
Katika uhai wake, Dk. Kyaruzi ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 alipata kuwa Katibu Mkuu wa Vyama vya Tanganyika African Association (TAA) na Tangayika African National Union (TANU), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanganyika katika Umoja wa Mataifa (UN), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF), Kanda ya Afrika, Kusini mwa Jwangwa la Sahara, akiwa na Makao yake Mjini Lagos, Nigeria.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amesema kuwa amehuzunishwa na kufadhaishwa na habari za kifo cha Balozi Kyaruzi ambaye alilitumikia Taifa la Tanzania na nchi nyingine kwa miaka mingi na kwa uaminifu,uadilifu na ufanisi mkubwa katika nafasi mbali mbali ambazo alipata kuzishikilia katika maisha yake.
“Nimepokea habari za kifo cha Mzee Kyaruzi kwa huzuni kubwa kwa sababu ya mchango mkubwa ambao aliutoa katika maisha yake kwenye utumishi wa taifa letu kuanzia kwenye nafasi za uongozi wa kijamii na kisiasa katika vyama vya TAA na TANU hadi kwenye utumishi wa Serikali huru ya Tanganyika na kwenye Umoja wa Mataifa,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake.
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Kagera salamu za rambirambi za dhati za moyo wangu kufuatia kifo cha Mzee Kyaruzi. Nakuomba pia kupitia kwako unifikishie salamu zangu kwa wana-familia wote wa familia ya Marehemu Kyaruzi.
Wajulishe kuwa niko nao katika wakati huu mgumu wa maombolezo. Naungana nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa. Nawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu, Naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze peponi pema roho ya Marehemu Vedasto Nshunju Kyaruzi. Amen.”