Mnyika afunika Dar es Salaam

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika akiwa amebebwa na Wafuasi wake baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumtangaza jana kuwa mshindi halali katika matokeo yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

AMBWAGA TENA MGOMBEA CCM, MAHAKAMA KUU YATUPILIA MBALI MADAI YA NGH’UMBI

NDEREMO na vifijo vya wapenzi na Chadema, jana viliitikisa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam baada ya Jaji Upendo Msuya kutupilia mbali madai ya aliyekuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Ubungo kupitia CCM, Hawa Ngh’umbi kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika wa Chadema.

Huu ni ushindi wa pili wa Mnyika dhidi ya Ngh’umbi baada ya kumshinda katika matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo hilo la Ubungo, katika uchaguzi wa Oktoba 31, 2010.

Katika hukumu hiyo ya kurasa 57 aliyoisoma kwa saa 1:21 (kuanzia saa 4:10 hadi 5:31), Jaji Msuya alitupilia mbali hoja zote tano, ambazo pande zote ziliyakubali kama mambo yaliyokuwa tata, hivyo kuhitaji uamuzi wa mahakama.

Jaji Msuya alitupilia mbali madai yote ya Ngh’umbi akisema ameshindwa kuyathibitisha mahakamani pasi na shaka, huku akidai kuwa ushahidi wa shahidi wa kwanza (PW10 upande wa madai) ulikuwa ni maneno ya kusikia tu ambayo hakuyashuhudia.

Ngh’umbi alifungua kesi dhidi ya Mnyika akidai kwamba uchaguzi huo uligubikwa na ukiukwaji wa taratibu wakati wa mchakato wa kampeni na utangazaji matokeo.

Mbali na Mnyika ambaye alikuwa mdaiwa wa pili katika kesi hiyo wadaiwa wengine walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni).

Katika kesi hiyo namba 107 ya mwaka 2010, Ngh’umbi ambaye alikuwa akitetewa na Wakili Issa Maige, katika hati yake ya madai na wakati akitoa ushahidi wake mahakamani pamoja na mashahidi wake alidai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria katika uchaguzi huo.

Ngh’umbi alidai kuwa, ukiukwaji wa sheria ulifanywa katika mchakato wa ujumlishaji wa kura na utangazaji wa matokeo, hivyo uliathiri matokeo ya uchaguzi huo kwa ujumla wake.

Kutokana na madai hayo, Ngh’umbi aliiomba Mahakama pamoja na mambo mengine ibatilishe matokeo hayo na kuamuru ufanyike uchaguzi mdogo.

Hata hivyo, katika hukumu yake Mahakama ilitupilia mbali madai na maombi yote ya Ngh’umbi na kumthibitisha Mnyika kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.

Katika hukumu hiyo, Jaji Msuya alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wachache na kwamba, mlalamikaji huyo alipaswa kuwaita mahakamani baadhi ya watu kutoka upande aliokuwa akiulalamikia kwenda kumtetea.

Chadema walipuka
Hukumu hiyo ya Jaji Msuya iliamsha shangwe kubwa, makofi na miluzi miongoni mwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika ndani na nje ya mahakama hiyo, wakifuatilia hukumu hiyo kupitia kwenye spika zilizowekwa nje ya ukumbi wa mahakama.

Wakati Chadema wakichekelea, upande wa mlalamikaji Ngh’umbi na Wakili wake, Maige walielezea kutoridhishwa na hukumu hiyo huku wakielezea kushangazwa na sababu alizozitoa Jaji Msuya kutupilia mbali madai yao na kumpa ushindi Mnyika.

Kwa upande wao wafuasi wa Chadema walielezea kuridhishwa na hukumu hiyo huku Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe ambaye pia alihudhuria mahakamani hapo akisema kuwa Mahakama imedhihirisha kuwa inatenda haki hata kwa wapinzani.

Katika hukumu yake, Jaji Msuya alisema anatambua kuwa wingi wa mashahidi si kigezo cha kushinda kesi ila kuaminika na kukubalika kwa ushahidi wa mashahidi.

Alisema mlalamikaji alishindwa kuithibitishia mahakama madai yake kwa kushindwa kuwaita mahakamani mashahidi wengi zaidi ili kuunga mkono ushahidi wa mashahidi wake wawili.

Baadhi ya mashahidi ambao Jaji Msuya aliwataja kwamba walipaswa kuitwa mahakamani na upande wa walalamikaji ni pamoja na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Lambart Kyaro na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Rajabu Kiravu.

CHANZO: Mwananchi kusoma zaidi habari hii bofya http://www.mwananchi.co.tz