Hatimaye Lyod Nchunga wa Yanga ajiuzulu

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Lyod Nchunga ametangaza kujiuzulu rasmi kwenye nafasi hiyo. Nchunga ametangaza uamuzi huo leo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari huku akisisitiza kuwa amechukua uamuzi huo ili kuinusuru Yanga.

Amesema uamuzi wake wa kujiuzulu kamwe usichukuliwe ni shinikizo la upande wowote, kwani bado anamapenzi na Klabu ya Yanga na atabaki kuwa mwanachama hai muda wowote.

Hata hivyo kujiuzulu kwa kiongozi huo aliyeibua mzozo ndani ya Klabu hiyo kumepokelewa kwa furaha na Wazee wa Klabu ya Yanga kwa kuwa tangu Yanga ipokee kichapo cha magoli matano bila toka kwa watani wao wa Jadi Simba hali imekuwa mbaya huku baadhi ya wanachama wakiwemo wazee wakimtaka kiongozi huyo kuachia ngazi.

Kujiuzulu kwa Nchunga kumekuja siku chache baada ya wanachama takribani 700 waliokutana jijini Dar es Salaam kumvua madaraka Nchunga kwenye mkutano huo, japokuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipinga uamuzi wa wanachama hao na kudai bado wanamtambua Nchunga.

Kufuatia kujiuzulu kwa kiongozo huyo madaraka na kuiongoza timu amekabidhiwa mdhamini mkuu wa timu ambaye ni Yusuf Manji, anayetarajiwa kusimamia zoezi la usajili wachezaji katika msimu mpya.