Ajali za barabarani zapungua mkoani Kilimanjaro

Ajali barabarani

Na Mwandishi Wetu, Moshi

MATUKIO ya ajali za barabarani katika Mkoa wa Kilimanjaro yamepungua kutoka 392 kwa mwezi Oktoba hadi Desemba 2011 na kufikia matukio 372 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.

Taarifa hizo zimetolewa jana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Kilimanjaro (RTO), Peter Sima wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake kuhusiana na hali ya ajali za katika mkoa huo.

Sima alisema kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu kumeonekana kuwa na upungufu wa ajali 20 ikilinganishwa na miezi mitatu ya mwishoni mwa mwaka jana 2011, na kwamba ajali za vifo ziliongezeka kutoka 40 hadi kufikia 43 huku za majeruhi zikipungua kutoka 159 hadi kufikia 153.

Akifafanua zaidi Kamanda Sima alisema katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi disemba mwaka 2011 matukio ya ajali yalikuwa 392 ambapo ajali za vifo zilikuwa 40, ajali za majeruhi 159 huku za kawaida ambazo hazikuleta madhara zikiwa 193.

Alisema kipindi cha Januari hadi machi mwaka huu matukio ya ajali yalikuwa 372 ambapo ajali za vifo zilikuwa 43,za majeruhi 153 huku za kawaida zikiwa 173.

Aidha alisema kupungua kwa matukio hayo kumetokana na elimu ya usalama barabarani ambayo wamekuwa wakiitoa mara kwa mara kwa wadau wa barabara ambayo inalenga usalama barabarani ili kuhakikisha wadau wote wa barabara wanafuata sheria na kanuni za barabara.

Aidha kamanda Sima alisema kufuatia hali hiyo jeshi la polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani kimejiwekea mikakati mbalimbali ya kupunguza matukio ya ajali za barabarani ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya barabara.

Alisema jitihada nyingine ambazo wanachukua ni kufanya doria kwa kutumia magari, pikipiki na hata kutembea kwa miguu ili kuweza kuwabaini watu wanaokiuka sheria za usalama barabarani pamoja na kutoa semina mbalimbali zinazolenga kuelimisha matumizi sahihi ya barabara kwa kushirikiana na wamiliki wa vyuo vya udereva mkoani hapa.

Katika hatua nyingine Kamanda Sima aliwataka watumiaji wote wa barabara kutambua kuwa ni wajibu wao kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kufanikisha malengo ya kupunguza matukio ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikisababisha watu wengi kupoteza maisha na hata wengine kupata ulemavu wa kudumu.

Aliwataka pia abiria kuhakikisha kuwa wawapo kwenye gari dereva wao yupo makini na anafuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dereva ni mzima na hajatumia kilevi chochote hatua ambayo itasaidia kuwaepusha na ajali badala ya kusubiri ajali itokee ndipo kuanza kushuhudia kuwa dereva alikuwa mlevi na alikuwa anakimbiza ga