Na Thomas Dominick
JESHI la Polisi Mkoa wa Mara limefanikiwa kupata silaha aina ya SMG nne na risasi 436 ndani ya wiki mbili baada ya kuwakamata watuhumiwa nane ambao wanasadikika kufanya uhalifu na uwindaji hasa katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Robert Boaz alisema kuwa jeshi hilo lilipata habari kuwa kuna mtu mmoja anamiliki silaha ndipo walikwenda katika kijiji cha Bisarara wilaya ya Serengeti na kumkamta Marwa Makoba (40).
“Baada ya kumkamata tulifanya upekuzi nyumbani kwake na kupata silaha mbili aina ya SMG na risasi 228 pia alipofikishwa kituoni tulifanya naye mahojiano kwa kina alisema kuwa anashirikiana na wenzake watano,” alisema Kamanda Boaz.
Kamanda Boaz alisema kuwa mtuhumiwa huyo aliwataja wenzake aliokuwa anashirikiana nao na ndipo askari walikwenda mjini Mugumu katika moja
ya nyumba za kulala wageni na kuwakamata watuhumiwa wengine ambao walitoka mikoa mbalimbali.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Fares Nazareti (37), Erasto Chubwa (46) wakazi wa Bukombe Geita, Magina Bathromeo (36) na Yohana Godfrey (30) wakazi wa Urambo Tabora, Japhet Bua (28), na Amosi Kagoma wakazi wa Kibondo, Kigoma.
“Tulipofanya nao mahojiano zaidi huyu amosi Kagoma alikubali kuwapeleka askari nyumbani kwao Kibondo na kuonesha SMG moja, naye Yohana Godfrey aliwapeleka askari Tabora na kuonesha silaha nyingine,” alisema.
Pia alisema kuwa katika tukio jingine lililotokea May 20 mwaka huu mtu
aliyejulikana kwa jina la Keringo Samara (30) baada ya kupekuliwa
alikutwa na risasi sita za SMG polisi wanaendelea na mahojiano nayeili
kubaini kama anamiliki silaha.
Kamanda Boaz alisema kuwa uchunguzi bado unaendelea na ukikamilika
watafikishwa mahakamani kujibu kesi inayowakabili ya kufanya vitendo
vya uhalifu na kukutwa na silaha kinyume na sheria.
Pia ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona kuna mtu
anamiliki silaha kinyume na sheria ili jeshi hilo liweze kuzikusanya
ili kupunguza vitendo vya ujambazi.