Polisi Arusha wataka wananchi kutojichukulia hatua mkononi

Kamanda wa Jeshi la Polisi Arusha, Thobias Andengenye

Na Mwandishi Wetu, Arusha

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, baada ya watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuuwawa na wananchi wenye hasira kali.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani
hapa SACP, Thobias Andengenye alisema kwua tukio hilo lilitokea Mei 22
mwaka huu majira ya saa kumi alfajiri huko Ngusero kata ya Sokon I
eneo la mwisho wa hiace.

SACP Andengenye alisema watu hao watatu ambao walikuwa ndani ya gari lenye namba za usajili T 830 AHU aina ya Toyota Mark II, ambao wanadaiwa kuwa walikuwa wakirandaranda katika eneo hilo jambo lililowatia hofu baadhi ya wananchi.

Alisema kuwa wananchi walizidi kupata hofu jambo lililowasababishia kuamshana na kulizingira gari hilo na kuanza kuwahoji watu hao ambao hawakuwapa maelezo ya kujitosheleza.

Inadaiwa kuwa wananchi hao walianza kuwashambulia watu hao kwa mawe na silaha za jadi na kufariki katika eneo hilo la tukio na wananchi hao walipofanya upekuzi katika gari hilo walikuta vifaa vya kuvunjia
milango.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Philip Naftal anayekadiriwa kuwa na
umri wa miaka 50-55, mwingine alifahamika kwa jina maarufu la Shidaa na wa tatu hakuweza kufahamika jina lake mara moja.

Alisema kuwa Jeshi hilo linaendelea kupepeleza waliohusika na mauaji
ya watu hao na iwapo watabainika watachukuliwa hatua za kisheria kwani wananchi hawapaswi kujichukulia sheri mikononi.

Kamanda alisema kuwa Philip na Shidaa ni moja ya watuhumiwa ambao jeshi hilo lilikuwa likiwasaka kwa kujihusisha na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuongeza kuwa hicho siyo kigezo cha kuwafanya wananchi kujichukulia sheria mikononi kwani kwa kufanya hivyo ni kufichua kosa kwa kufanya kosa.