Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro
KITUO cha Maendeleo ya Viwanda mkoani Kilimanjaro (KIDT) kinakabiliwa na uchakavu wa mashine na ukosefu wa mitaji hali inayosababisha kituo kishindwe kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija.
Kutokana na changamoto hizo, kituo hicho kinahitaji zaidi ya sh. milion 800 kwa ajili ya maboresho na mtaji ili kuweza kulikabili soko na kuingia katika ushindani.
Hayo yalibainishwa na Meneja Mkuu wa Kituo hicho, Frank Elisa wakati akizungumza na waandishi wa habari hizi ofisini kwake kuhusiana na hali ya uzalishaji katika kituo hicho pamoja na changamoto zinazowakabili.
Elisa alisema katika kituo hicho ambacho kinaviwanda vinavyotengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo vikombe vya kuunganishia nyaya za umeme (Insulator), vyombo vya udongo vya nyumbani kama sahani na vikombe, kuni, matofali, Fanicha na nyinginezo kinakabiliwa na changamoto kuwa ya uchakavu wa mitambo hali inayosababisha mahitaji kuwa makubwa ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji.
“Katika kituo hiki tumekuwa tukijitahidi sana katika uzalishaji, lakini tatizo kubwa ni mitambo mingi kuwa chakavu na ya kizamani, na soko la bidhaa hizi ni kubwa sana kwani kama insulator tunazotengezeza zote zinaoda Tanesco, na pia ziko nchi nyingine za nje ambazo zimekuwa zikihitaji bidhaa hii lakini tumeshindwa kutokana na uwezo wetu wa kuzalisha kuwa mdogo,” alisema Elisa.
Kufuatilia hali hiyo, Elisa aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kiuboresha viwanda vilivyopo katika kituo hicho ikiwemo cha utengenezaji Insulator na vyombo ili kuweza kukuza uzalishaji na kufanikiwa kusonga mbele kimaendeleo na kuinua soko la ajira hapa nchini kupitia viwanda.
Alisema bila viwanda hakuna maendele wala ajira, hivyo ni vema Serikali ikawekeza katika viwanda na kuangalia kwa makini viwanda vilivyopo ili kuhakikisha vinafanikisha adhma ya kuinua nchi kiuchumi na kukuza soko la ajira.
“Serikali iangalie namna ya kuboresha viwanda vilivyopo ingwa ni vichache na vidogo, kwani fursa za kupiga hatua kimaendele zipo na wateja ni wengi sana hasa kwenye vifaa hivi ambavyo vinahitajika Tanesko na tumekuwa tukipata pia tenda za Nje lakini tatizo ni kwamba uzalishaji wetu ni mdogo, Serikali iliangalie hili kwa umakini wake kwani viwanda hivi vitasaidia uchumi wetu katika mkoa wa kilimanjro na Taifa kwa ujumla kutaimarika na vijana wengi kupata ajira katika viwanda hivyo,” alisisitiza Elisa.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kituo cha KIDT wilayani Same, ambacho kinahusika na utengenezaji wa Insulator na vyombo vya udongo na jamii yake Loveness Mhina aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha vitendea kazi katika kituo hicho ili kuwawezesha kuingia katika ushindani wa soko la jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhina aliwataka pia watanzania kujijengea tabia ya kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini hatua ambayo itawezesha kukua kwa ushindani na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Ushindani wa soko katika bidhaa tunazozalisha ni mkubwa sana, tunaiomba serikali itutupie macho ili kutuwezewsha kukabiliana na changamoto kubwa ya ushindani inayotukabili kwa sasa, na endapo Serikali itaboresha vitendea kazi kwa kweli tutapiga hatua kubwa sana katika uzalishaji, lakini katika hili pia nawasihi watanzania wenzangu waache tabia ya kupenda bidhaa za nje ya nchi kwa kisingizio kuwa ni imara na badala yake wapende za hapa nchini kwani hata ukifuatilia utakuta za kwetu ni imara zaidi,” alisema Mhina.