Na mwandishi wetu,
Musoma
MKUU wa Mkoa wa Mara John Tuppa amewataka watendaji ndani ya Mkoa huo kuwabana mawakala wa ruzuku za pembejeo za kilimo ambao wanakwenda kinyume na makusudio ya Serikali.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni baada ya kupata taarifa kuwa kuna mawakala walichukua vocha za pembejeo zilizoandikwa majina ya wakulima na kupeleka kwenye shule na kuwapa wanafunzi wazisaini ili fedha zake wazitafune bile kupeleka kwa wakulima.
“Hizi ni tabia za kinyama ambazo hatuwezi kuzivumilia hata kidogo hivyo ninyi watendaji wa Serikali ebu simamieni hizi fedha za Umma ziweze kuwanufaisha na kuboresha maisha ya wananchi wetu,”alisema Tuppa.
Alisema kuwa mpango wa serikali kwa sasa ni kuwainua wananchi wake kupitia kilimo kwa kutoa ruzuku za kilimo ili kiwe cha kisasa ambacho kitawapatia faida wananchi wake na si kuwanufaisha watu wachache.
“Hivi sisi watendaji wa serikali tunalipwa mishahara kwa lipi kama hatutaki kusimamia majukumu yetu hasa haya ya wananchi ambao wanapata taabu kwa kuibiwa na mawakala ambao sio waaminifu sasa tujitume na kuwabana hawa ili wananchi wetu wanufaike na Serikali yao,”alisema.
Alisema kuwa halmashauri iliyofanya vizuri kati ya sita za Mkoa huo ni halmashauri ya Tarime wakati, Bunda, Musoma mjini, Musoma vijijini, rorya, Serengeti zimefanya vibaya wakati kuna kamati za kusimamia zoezi hilo.
“Serikali yetu inatoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya wananchi hasa katika kilimo lakini kuna watu wachache ndio wanajiona wana haki ya kunufaika nazo wakati kuna watendaji na kamati zinazoteuliwa kwa ajili ya kusimamia fedha hizo,”alisema.
Alisema kuwa kutokana na vitendo hivyo watendaji hao hawaitendei haki serikali yao ambayo wameajiriwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wao pamoja na kutatua kero za aina hizo.