Na Mwandishi Maalumu, Washington DC
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameupongeza uongozi wa Tawi la CCM Washington kwa juhudi wanazofanya hasa katika kipindi hiki ambacho kimeuwezesha uongozi kufungua tawi na kupata wanachama 250 katika Miji ya DC, Maryland na Virginia.
Mwenyekiti wa CCM ametoa pongezi hizo kwa viongozi hao walipofika kujitambulisha na kumsalimia Mwenyekiti wao katika hoteli ya Ritz-Carlton.
“Nawapongeza sana kwa juhudi zenu mnazofanya hadi kufungua tawi hapa Washington hasa katika kipindi hiki ambacho kina changamoto nyingi” Mwenyekiti amewaeleza viongozi hao ambao ni Mwenyekiti Bi Loveness Mamuya, Katibu Bw. Jacob Kinyemi na Katibu Mwenezi, Givens Kisanji.
Viongozi hao ambao wamefuatana na Katibu wa Tawi la New York Bw. Shaban Mseba wamemueleza Mwenyekiti kuwa tawi lao limefunguliwa rasmi mwezi Novemba, mwaka 2011. Akisoma risala kwa Mwenyekiti wa CCM, Kinyemi amesema tawi lao, pamoja na kuwa ni changa, linakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa na kiuchumi.
Bw. Kinyemi ameeleza madhumuni na malengo ya Tawi la CCM mjini Washington kuwa ni pamoja kuwawezesha wanachama wake kupata mitaji , kuitangaza Tanzania, kupata elimu, biashara na kusaidia katika kutafuta wabia na wenza wa maendeleo katika kuendeleza nchi na watu wake kiujumla.
Mwenyekiti Kikwete amewaasa wanachama hao kusimama kidete katika kukitetea, kukipigania na kujivunia mafanikio ambayo serikali ya CCM imeyafikia na kuyatimiza.
Amewakumbusha hatua kubwa ambayo serikali ya CCM imepiga hatua katika elimu, afya, kilimo na miundombinu na kuwaasa wanachama hao kujivunia mafanikio hayo na kuupuuza maneno ya wapinzani wa CCM, ambayo nia yao ni kuwakatisha tamaa wananchi.
Mwenyekiti wa CCM amewaeleza viongozi kuhusu changamoto zilizopo katika maeneo mbalimbali na kuahidi kuzishughulikia na hatimaye kuzimaliza changamoto zote. Rais Kikwete aliondoka Washington Mei 20, 2012 jioni na kuwasili Dar es Salaam, Mei 21, 2012.