TGNP kufanya mafunzo ya uraghibishi mikoa mitatu

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya

Na Mwandishi Wetu

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) unatarajia kufanya mafunzo ya uraghibishi ngazi ya jamii kwa mikoa mitatu ambayo ni Shinyanga, Morogoro na Mbeya, ambapo zoezi litafanyika katika wilaya za Mbeya vijijini, Morogoro Vijijini na Kishapu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya amesema mafunzo hayo yanatarajia kuanza Mei 22 hadi June 2, 2012.

Bi. Mallya alisema mafunzo hayo yana nia ya kuwajengea wananchi uwezo wa kushiriki, kuchambua kwa kina fursa na changamoto zinazowakabili katika mazingira yao na kuyatafutia ufumbuzi kwa kujenga vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

“Matarajio ya matokeo makubwa ya Mafunzo ya Uraghibishi na utafiti shirikishi wa kijamii, yatawashirikisha wanawake na wanaume walioko pembezoni katika kutambua fursa walizonazo katika kudai au kuingizwa kwa madai yao katika mchakato wa Katiba mpya, kudai mabadiliko ya sera, kimfumo, na haki ya uchumi kwa makundi yaliyoko pembezoni.”

“Mafunzo haya pia yatawajengea wanajamii uwezo wa kushiriki ipasavyo katika mchakato wa kutoa maoni kwa Tume ya Kuratibu Mchakato wa katiba mpya, haki ya uchumi, na maisha endelevu kwa wote.”

Aidha aliongeza baada ya mafunzo haya, wanajamii wataibua vipaumbele vya changamoto zinazowakumba na watajadili namna ya kukabiliana nazo wakiwa na viongozi wa serikali ngazi ya wilaya,kata na vijiji.

“Mwisho TGNP itaendesha warsha kwa wanajamii namna ya kuanzisha na kusimamia vituo vya taarifa na maarifa katika wilaya zao ikiwa ni sehemu ya kukutana na kushirikishana uzoefu na kujadili masuala mbali mbali zinazowakabili,” alisema Mallya katika taarifa yake.