Dk Shein: Changamoto za wananchi zitapatiwa ufumbuzi

Na Mwandishi Wetu
Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa miongoni mwa vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ni kuhakikisha changamoto zilizopo kwenye sekta za maji, umeme na huduma nyengine za kijamii zinapatiwa ufumbuzi haraka.

Dk. Shein aliyasema hayo jana mjini hapa kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wakulima pamoja na wakazi wa Wilaya ya Kusini Unguja katika ziara yake Wilaya ya Kusini Unguja.

Akizungumza na wananchi maeneo hayo, Dk. Shein aliwaahidi kuwa tatizo la huduma za maji na umeme tayari yameanza kufanyiwa kazi na yatamalizika muda si mrefu.

Alieleza kuwa ahadi zilizotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni kuhusiana na huduma muhimu ikiwemo maji na umeme zinafanyiwa kazi na wananchi watahakikishiwa makazi yao kuwa ya kisasa na bora zaidi.

Alieleza kuwa kutokana na kumalizika kwa mradi huo mkubwa wa maji alioutembelea, sasa juhudi zinahamia eneo lingine, ambapo ni kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi na kuondoa tatizo la maji kwa wakazi wa maeneo hayo.

Kwa upande wa huduma ya umeme, Dk. Shein alisema kutkana na huduma hiyo pia kuonekana ya lazima na si anasa kama ilivyokuwa siku za nyuma, amewaahidiwananchi wa Uswiswi kuwa huduma hiyo itawafikia hivyo kuwataka waanze kujiandaa. “Sasa mkae mkao wa kula,” alisema Dk. Shein.

Aidha aliwataka wananchi wanaoishi makazi mapya kujenga kwa kufuata utaratibu wa kisasa ili dharura inapotokea kwenye makazi yao iwe rahisi vyombo vya msaada kuingia na kuondoa hatari hiyo. “Tuhakikishe tunajenga na kuacha nafasi za viwanja vya michezo, maeneo ya shule, kituo cha afya na huduma nyingine muhimu za kijamii,” alisisitiza Dk. Shein.

Akiwa Uswiswi aliahidi kutoa mchango wa kuchimba kisima katika msikiti wa eneo hilo la makazi mapya ya Uswiswi na kupitisha harambee kwa viongozi aliofuatana nao ambao nao walicha fedha taslimu pamoja na ahadi kufikia zaidi ya milioni moja ambazo alishauri zitumike pia katika ujenzi wa msikiti.

Dk. Shein katika ziara hiyo pia alitembelea tanki la maji Kizimkazi Mkunguni na kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango Sera na Utafiti wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ayoub Mohamed, ambapo aliarifiwa kuwa mradi huo wa maji unaendelea vizuri.

Alisema kuwa mradi huo ambao ulianza mwaka 2007 na kugharimu zaidi ya milioni 350, mara utakapomalizika unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wapatao 5,000 wa maeneo hayo.

Maeneo mengine ambayo Dk. Shein aliyatembelea ni pamoja na Hospitali ya Makunduchi na leo anatarajia kumaliza ziara yake katika Mkoa wa Kusini Unguja na kufanya majumuisho ya ziara yake ya Mkoa wa Kusini.