Ziara ya Mama Salma Kikwete Washington DC

Mama Salma Kikwete akimsikiliza Dk. Nasra Nirza, daktari bingwa wa watoto wa Hospitali ya National Children kuhusu huduma wanayotoa kwa watoto wanaolazwa kwenye hospitali hiyo. Pembeni ya Mama Salma ni Dk. Hadija Mwamtemi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili alieyeongozana na Mama Kikwete kwenye ziara hiyo.

Mama Salma Kikwete akisisitiza jambo alipokuwa kwenye mkutano na wenyeji wake wa Hospitali ya Watoto National Children baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo.

Mama Salma Kikwete akimkabidhi maelezo kuhusu WAMA Mkuu wa Utawala wa Africare, Bi. Diana White kama ishara ya kuanzisha ushirikiano na taasisi hiyo ili kuendelea kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu masuala ya lishe Tanzania.

Na Mwandishi Maalumu, Washington DC

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amewahimiza wadau afya na lishe kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na taasisi za Kitanzania na Serikali kwa ujumla ili kuinua afya ya mtoto na mama nchini Tanzania.

Mama Salma aliyasema hayo alipokuwa kwenye mkutano wa pamoja na NGO sita za kimarekani zinazofanya kazi mbalimbali nchini Tanzania kwenye masuala ya lishe na afya tarehe 18 Mei 2012. Taasisi zilizohudhuria mkutano huo ni Malaria No More, Health Overseas Volunteers, Path International, Save the Children, Global Health and Diplomacy na Africare International, uliofanyika pembezoni na mikutano ya Rais Kikwete kuhusu masuala ya usalama wa chakula na lishe duniani.

Katika hotuba yake na taasisi hizo, Mama Salma Kikwete alizishukuru
taasisi hizo kwa kufanya kazi Tanzania ili kusaidia taifa kufikia malengo
yaliyowekwa kwenye dira ya taifa kuhusu masuala ya afya. Alihimiza
ushirikiano na taasisi nyingine za Kitanzania hususan kwenye masuala ya uhamashaji, utoaji wa elimu na kujenga uwezo kwa Watanzania kwenye masuala ya lishe.

Profesa Jerome Paulsen, Daktari na Mkurugenzi wa Children's Hospital Global Affairs akizungumza na ujumbe wa Mama Salma Kikwete kuhusu mpango wa Hospitali hiyo ya kuwafundisha madaktari kuhusu magonjwa ya watoto yatokanayo na uchafuzi wa mazingira.


Akijibu swali la mtaalamu wa usalama wa chakula na lishe kutoka USAID Bi. Laura Birx, Mama Salma Kikwete alisema msaada mkubwa unaohitajika kwa Watanzania ni rasilimali fedha na elimu ili kuinua hali ya lishe kwa watoto wa Tanzania.

“Kwenye maeneo mengi mjini, elimu kuhusu lishe ni muhimu zaidi kwani
baadhi ya familia wanauwezo wa kifedha na wanachohitaji sana ni elimu
kuhusu lishe,” Alisema Mama Kikwete.

Hii inatokana na hali ya maisha ya mjini ambapo wazazi wengi wanajikita na kazi na kuacha walezi wa nyumba kufuatilia lishe ya watoto. Alisema elimu kwa walezi hao ni muhimu sana ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanapewa lishe bora.

Hivi karibuni USAID kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya
kiserikali imetoa fedha $ 30 milioni kutekeleza mpango wa lishe Tanzania.
Mpango huo ujulikanao kama Mwanzo Bora Nutrition Program unatekelezwa kwenye mikoa mitatu ya Manyara, Morogoro na Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano. Mpango huo utakapokamilika utasaidia Serikali kujenga uwezo wa kutoa elimu kuhusu lishe, kuinua hali ya lishe ya watoto wadogo, wakina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

Mkutano wa Mama Salma Kikwete na taasisi hizo ulioratibiwa na Africare kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Marekani, umefungua milango ya ushirikiano baina ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na taasisi hizo sita ili kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa afya bora na lishe kwa watoto.

Kwenye ziara hiyo, Mama Kikwete na ujumbe wake pia walitembelea Hospitali Kuu ya Watoto Washington DC ya Children’s National Medical Center na kutembelea wodi ya watoto wenye mahitaji maalum.

Wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi wa Hospitali hiyo kwenye masuala ya Uhusiano ya Kimataifa Dk. Jerome Paulson alikubaliana na Dk. Hadija Hemedi Mwamtemi, Mkuu wa Idara ya Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuanza mazungumzo ya kushirikiana kwenye kuelimisha walimu (Training of trainers) watakaofundishwa wengine kuhusu afya ya msingi kwa watoto ili kujikinga na magonjwa yatokanayo na uharibifu wa mazingira.

Dk. Paulson alisema mpango huo wa kutoa elimu kwa watoa huduma ya afya kwa watoto hauna gharama kubwa lakini matunda yake yataonekana kwa kuwa na watoto wenye afya bora baada ya kuwalinda na magonjwa kama vile pumu yatokanayo na uchafuzi wa hewa.

Kwa upande wake Mama Salma Kikwete aliwasihi washirikiane na Chama chaMadaktari wa Watoto Tanzania (PAT) na Hospitali ya Taifa ya Taifa ya Muhimbili ili kwa pamoja kuanzisha mpango huo wa kubadilishana zoefu na kupeana ujuzi (TOT) ili kulinda afya ya watoto wa Tanzania. Mama Salma Kikwete alifanya ziara hiyo wakati Rais Kikwete akihudhuria Mkutano wa mwaka kuhusu Kilimo na Usalama wa Chakula Duniani Washington DC, Marekani.