Maafisa feki wa Ustawi wa Jamii wajitokeza

baadhi ya wanachuo wa chuo cha ustawi wa jamii katika moja ya maafali chuoni kwao

Na mwandishi wetu Kilimanjaro
WIMBI kubwa la watu walioibuka mitaani na kujiita wataalamu wa Ustawi wa jamii ili hali hawana taaluma ya fani hiyo wamejitokeza na kusababisha ongezeko la Maafisa ustawi wa jamii wasio na sifa.
Hayo yameelezwa na Naibu katibu wa chama cha maofisa ustawi wa jamii Tanzania (Taswo) Tawi la Kilimanjaro Bw. Elirehema Kaaya ,wakati wa mkutano wao mkuu wa mwaka uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi, ambapo alisema fani ya Ustawi wa jamii kwa sasa imevamiwa na watu mbalimbali ambao hawana taaluma wala sifa ya fani hiyo.
Bw. Kaaya alisema Watu hao ambao hawana taaluma ya Ustawi wa jamii wamekuwa wakijifanya maofisa ustawi wa jamii na kuanzisha vituo mbalimbali vya malezi ya watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu, kwa madai ya kuwasaidia huku lengo likiwa ni kujinufaisha binafsi hali ambayo alisema isipodhibitiwa vikali itaathiri kwa kiasi kikubwa fani hiyo.
“Fani hii ya ustawi wa jamii kwa sasa imevamiwa sana na watu wasio na taaluma,na watu wengi wameingia katika tasnia hii kwa lengo la kutafuta fedha na watu hawa badala ya kuisaidia jamii wanakuwa wanaiumiza, hii ni changamoto kubwa sana inayotukabili katika tasnia hii kwani hali hii imekuwa ikisababisha hata sisi ambao ni taaluma yetu kudharaulika katika jamii”alisema Bw. Kaaya.
Katika hatua nyingine Bw. Kaaya alisema tatizo la utelekezaji wa watoto hususani wale wenye ulemavu bado ni kubwa katika mkoa wa Kilimanjaro hali ambayo imekuwa ikisababisha makundi hayo kukosa haki zao za kimsingi ikiwemo elimu.
Aidha Bw. Kaaya aliishauri serikali katika suala la sense ya watu na makazi kuweka kipaumbele kikubwa kwa watu wenye ulemavu hasa watoto ili kuwezesha kupatikana kwa takwimu sahihi za watu hao kutokana na kwamba hadi sasa takwimu za kundi hilo ni changamoto kubwa katika serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taswo mkoani Kilimanjaro Bi. Agness Urassa alisema kwa sasa kunaupungufu mkuwa wa wataalamu wa ustawi wa jamii hali ambayo inasababisha kuwepo kwa utendaji duni katika jamii.
Bi. Urassa alisema shirika hilo limeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha jamii inapata huduma bora kupitia wataalamu wa ustawi wa jamii waliopo lengo likiwa ni kupunguza matatizo mbalimbali yaliyoko ndani ya jamii.
Naye Ofisa ustawi wa jamii sekretarieti ya mkoa wa Kilimanjaro Bw. Sammy Muleba aliitaka jamii kuondokana na dhana potofu kuwa watoto wenye ulemavu si wakawaida na badala yake iamini kuwa ni watoto kama watoto wengine hivyo waache kuwaficha ndani na wahakikishe wanapata haki zao zote za kimsingi.