Na Mwandishi Wetu
Tarime
MBUNGE wa Jimbo la Singida Kusini kupitia CHADEMA, Tundu Lissu na wezake saba jana waliachiwa baada ya kupata dhamana ya masharti matatu likiwemo la kusaini hati zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 70.
Mbali na Lissu watuhumiwa wengine waliofikishwa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime kwa kesi no. 210 ya mwaka 2011 ni mkurugenzi wa utafiti na sera wa chama hicho Mwita Waitara ambapo kila alitakiwa kudhaminiwa na watu wawili wakazi wa tarime kwa kusaini hati ya milioni tano kila mmoja.
Aidha masharti mengine ambayo yalitolewa mahakamani hapo ni pamoja na washitakiwa hao kudhamiwa na wenyeji wa wilaya hiyo wanaoaminika ama kuwa na hati ya mali isiyohamishika ambapo watuhumiwa wote walitimiza masharti.
Hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Tarime Yusto Ruboroga alitoa sharti lingine kwa washitakiwa katika kesi hiyo kwa kuwataka watuhumiwa hao wote kutofika eneo la Nyamongo wakati wote ambapo kesi hiyo inaendelea.
Ndani ya viwanja vya mahakama jeshi la polisi lilihimarisha ulinzi wakati wote hadi mahakama ilipotoa dhamana kwa washitakiwa hivyo kuruhusu polisi walikuwa na kila aina ya silaha kupata nafasi ya kupumua.
Wananchi waliokuwa katika eneo hilo walishangaa kuona ulinzi ukiwa mkali katika eneo hilo huku wakihoji kwanini ulinzi kama huo usitumike kulinda rasilimali ambazo kila kukicha zinaleta malumbano kwa Watanzania.
Katika kesi hiyo mbali na Mbunge wa Singida Kusini, watuhumiwa wengine ni mwita Waitara, Ibrahim Juma Kimu(27) mkazi wa Sabasaba Singida ambaye ni dereva wa Lisu,Bashir Seleman(35)mkazi wa Sterehe Tarime Stanslaus, Nyembea(33) mkazi ubunge msewe Dar es salaam,Andasn Chacha(35) mkazi wa Ronsoti tarime,Andrew Nyandu(63)mkazi wa Mang’onyi Singida,Mwita Marwa(48)mkazi wa Bonchugu Serengeti.
Akizungumza baada ya dhamana, Lissu alisema hatua ya yeye kuingia gerezani imemwezesha kujua unyanyasaji mkubwa unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wananchi ikiwa ni pamoja na kubambikiziwa kesi.
“Kitendo cha mimi kwenda gerezani nimejua mambo mengi ikiwemo unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya dola na watu kupewa kesi,” alisema Lissu
Katika mahakama hiyo ilidaiwa kuwa mei 23 majira ya saa 4 usiku washitakiwa wote kwa pamoja waliingia kwa jinai katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti,kufanya mkusanyiko eneo hilo la hospitali bila ya kibali na kuzuia uchunguzi wa miili ya marehemu kinyume cha sheria.
Hatua hiyo inafuatia mauaji ya risasi yaliyofanywa na Jeshi la Polisi eneo la Nyamongo wilayani Tarime ambapo inadaiwa kuwa takribani zaidi ya watu 800 walitaka kuvamia mgodi wa North Mara-Barrick na katika mapambano na polisi watu watano waliuawa na wengine nane kujeruhiwa.