CCM wameteka Mchakato wa Katiba-Chadema

Mh. John Mnyika, Mbunge wa Ubungo na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeijia juu Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) kwa kitendo cha kuteka mchakato wa katiba mpya kabla ya wananchi kutoa maoni yao na kusisitiza kuwa suala hilo haliwezi kukubalika.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kushangazwa na taarifa za kikao chao cha NEC hivi karibuni ambazo zinaeleza kuna baadhi ya vipengele havitafanyiwa marekebisho katika katiba mpya.

Alisema suala hilo limejionyesha dhahiri kuwa CCM inataka kuchakachukua mchakato wa katiba kabla ya wananchi kutoa maoni yao na kwamba suala hilo litasababishia kupatikana kwa katiba mbovu jambo ambalo hawatalikubali.

Mnyika alisema CCM haina dhamira ya kupata katiba mpya ndio maana wameanza kueleza kuwa kuna baadhi ya vipengele havitaguswa.

“Mchakato wa katiba sio wa CCM peke yao ni wa Watanzania wote na kama wameanza kusema kuna maeneo hayataguswa katika katiba hiyo mambo yatabaki kuwa pale pale ina maana hatutapata katiba mpya tutapata ambayo imefanyiwa marekebisho ni lazima wafuate maoni ya wananchi na sio ya CCM,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, alisema wanachokihitaji ni katiba mpya na sio maboresho ya suala hilo na kila raia ana wajibu wa kutoa maoni yake katika mchakato huo.

“CCM imejifungia kwenye NEC na kuanza kueleza kuna mambo ambayo hayatabadilika kwenye katiba hiyo, hilo hatuwezi kulikubali ni lazima kuwepo na ridhaa ya watu kwa kusikiliza maoni ya wananchi na sio kuanza kueleza kuna mambo ambayo hayataguswa.

Mnyika alisema ukiangalia kwa sasa Serikali imepoteza uhalali katika masuala ya ardhi hali ambayo inasababishia kuwepo na migogoro ya mara kwa mara.

Hata hivyo, akasema Chadema imejipanga kikamilifu katika kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya mchakato wa katiba mpya na kwamba ifikapo Mei 26, mwaka huu watafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema baada ya hapo ifikapo Mei 28, mwaka huu watafanya operesheni ya kanda ya Kusini kwa kwa siku 15 mfululizo jimbo kwa jimbo mpaka kieleweke lengo ni kuunganisha nguvu ya umma, kujadili changamoto zinazoikabili taifa pamoja na kujenga oganizesheni ya chama.

Mnyika alisema katika mikutano hiyo wataenda kuibua mjadala mkubwa kuhusiana na mchakato wa katiba mpya na kwamba CCM iwaache watanzania wachague wanachokitaka katika katiba hiyo na sio kuanza kuichakachua.

Alisema ameshangazwa na kauli ya NEC kuhusiana na kupanda kwa gharama za maisha ambapo walieleza mahindi yametolewa, mchele na sukari lakini watu wamekuwa wakiyasafirisha na kuyauza nje ya nchi.

Mnyika alisema hata katika sherehe za Mei mosi, Rais Kikwete alizungumzia suala hilo kuwa kuna mahindi yamesafirishwa nje ya nchi na kuuzwa badala ya kueleza ni hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya hao wanaohusika kufanya suala hilo.

“Ni kwa nini hawaelezi hatua zinazochukuliwa dhidi ya waliohusika kwa ajili ya kuuza bidhaa hizo kauli yao imejionyesha wanachama dhaifu na viongozi wake ni dhaifu,” alisema Mnyika.

Alisema kwa sasa chama chake kimeweka mikakati ya kuing’oa CCM madarakani kwani chama hicho kimetekwa na mafisadi.

Akizungumzia sakata la Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, alisema kuwa tayari kamati kuu ya chama ilikutana na kufanya maamuzi dhidi yake kwa kauli alizokuwa akizitoa kipindi cha nyuma na kumpa onyo kali.

CHANZO: NIPASHE