Hali si shwari CCM Arusha

Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Arusha, James ole Millya


Hili ni tamko la baadhi ya wajumbe wa UVCCM Arusha

Ndugu zangu waandishi wa habari leo tumeona tuwaite hapa ili tuweze
kutoa maoni yetu kuhusiana na mustakabali wa chama chetu cha Mapinduzi
na Jumuiya yetu ya Umoja wa vijana wa CCM mkoa wa Arusha.
Tumewaita hapa kwa malengo makuu Sita:-
Kuunga mkono Halimashauri kuu ya CCM Taifa kwa kuona umuhimu wa
kuifanyia kazi kwa vitendo falsafa ya kujivua gamba. Tunaipongeza na
kuiunga mkono Halmashauri kuu ya CCM Taifa kwa kutambua kwamba
mafisadi wamechangia sana kukidhoofisha na kukipotezea mvuto chama
chetu mbele ya umma wa watanzania. Kwa mantiki hiyo tunatamka kwa
kauli moja kwamba mapacha hao watatu wa kifisadi ambao ni Edward
Lowasa, Rostam Azizi na Andrew Chenge na vibaraka wao wafukuzwe mara
moja kwa maslahi ya CCM na Watanzania. Pia tunasisitiza kuwa Andrew
Chenge aondolewe kwenye kamati ya maadili ya CCM mara moja na wakati
huohuo Edward afukuzwe kwenye kwenye ya uwenyekiti wa Bodi ya udhamini
ya umoja wa vijana wa CCM Taifa haraka iwezekanavyo.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha
tunamtaka kuwa James Millya ambaye ni kibaraka mkuu wa mafisadi mkoa
wa Arusha ajiuzulu mara moja na tunatamka rasmi kumfukuza kwenye UVCCM
mkoa wa Arusha ili apate fursa ya kwenda kuwa tumikia mafisadi.
Tunamtaka James Millya aache kufikiria kwa kutumia tumbo na badala
yake atumie kichwa. Pia tumeshaandika barua yenye kumbukumbu namba
kumb. Ars/Malalamiko/01 kwenye Chama kuelezea namna alivyo mnafiki,
mfitini,mwongo na namna asivyo jali maslahi ya vijana wa UVCCM mkoa wa
Arusha. Vilevile tunapenda kuujulisha umma wa Tanzania kuwa Ally
Bananga anaetumiwa na Millya pamoja na mafisadi hana nafasi yoyote
ndani ya Umoja wa vijana wa CCM kuanzia kwenye tawi hadi Taifa. Kwa
mantiki hiyo Ally Bananga aache mara moja kuganga njaa kwa kutumia
jina la UVCCM. Pia tunampa onyo kali Catherine Magige aache mara moja
kutumia fedha za mafisadi kuwagawa vijana wa Arusha kabla hatujatumia
haki yetu ya kikanuni ya kumsimamisha Ubunge. Tunajua kuwa amepata
ubunge kwa nguvu za kifisadi kupitia UVCCM.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha
tunakiomba chama cha cha mapinduzi kiwafukuze mara moja makatibu wa
UVCCM kutoka wilaya za Monduli, Arumeru, Longido na Karatu kwa
kushiriki mandalizi ya maandamo haramu na kwa kukataa wito wa chama wa
kwenda kutoa ushahidi wa malamiko yao kuhusu mjumbe wa Baraza kuu la
UVCCM Taifa. Kitendo hicho cha kukataa wito wa Chama ni dharau na
ukosefu wa maadili.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha
tunatamka kwamba ili kulinda hadhi ya CCM mkoa wa Arusha tunamtaka
Onesmo Nangole ajiuzulu mara moja kwa kuwa anafanya kazi ya Fisadi
Edward Lowasa na si ya CCM. Kitendo chake yeye cha kufanya kazi ya
mafisadi na si ya CCM kimetupelekea kupoteza majimbo mawili kwenye
uchaguzi mkuu wa 2010.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha
tunatamka kwamba Mhe. Mary Chatanda (MB) ambaye ni katibu wa CCM Mkoa
wa Arusha ni mpiganaji na ni lulu ya CCM mkoa wa Arusha. Amefanya
mengi ya maana na wa-CCM makini, wazalendo na wanaojali maslahi ya
chama chetu wanatambua hilo. Pia tunawaomba CCM Taifa waendelee
kumwacha hapa Arusha ili aendelee kukijenga chama na kukomesha
mafisadi pamoja na dagaa wao.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha
tunatamka rasmi kumtambua Ndugu. Mrisho Gambo kuwa ni mjumbe halali wa
baraza kuu la UVCCM Taifa kuwakilisha mkoa wa Arusha. Tunamuunga mkono
kwa ujasiri wake, umahiri wake na uzalendo wake wa kupambana na
ufisadi ndani ya chama na Tanzania kwa ujumla. Na huo ndiyo msimamo
wetu kwa kuwa una tija kwa vijana wa Tanzania. Tunashauri CCM Taifa
kuwaita rasmi mapacha watatu wa kifisadi (Edward Lowasa, Rostam Azizi
na Andrew Chenge) kwenye kamati ya maadili ya CCM Taifa na kisha
kuwafukuza mara moja kama kweli tuna nia ya kuendelea kuwa chama
tawala katika nchi hii.

TUTASEMA KWELI DAIMA FITINA KWETU MWIKO
KAULI YETU: KULINDA NA KUJENGA UJAMAA
KITADUMU CHAMA CHA MAPINDUZI BILA MAFISADI